WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika imetangaza kuingia nchini
kwa ugonjwa hatari wa mahindi ujulikanao kitaalamu kwa jina la maize
lethel necrosis (MLND.
Septemba mwaka jana wizara hiyo ilitoa taarifa kwa umma kuhusu ugonjwa
huo baada ya kupata taarifa kwamba ugonjwa huo umegundulika kuwepo
katika eneo la Bornet-Kenya.
Taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa huo nchini ilitolewa jana kwa kupitia
vyombo vya habari na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika,
Mohamed Muya, na kwamba tayari umeanza kuonekana katika wilaya ya
Bariadi, mkoa wa Simiyu, na Babati, mkoa wa Manyara.
Kwa mujibu wa Muya ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vijulikanavyo
kitaalamu kama maize chlorotic mottle (MCMV) na sugarcane mosaic (SCMV)
umegunduliwa nchini na wataalamu wa wizara baada ya kufuatilia mwenendo
wa ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kasi ya mashambulizi ya ugonjwa huu na uharibifu unaweza kuwa mkubwa
kiasi cha kufikia hadi hasara ya asilimia 100. Mahindi yaliyoshambuliwa
huwa na magunzi madogo na maumbile yasiyo ya kawaida; pengine yanakuwa
na mbegu chache au yasiweke mbegu kabisa,” ilisema taarifa ya wizara ya
kilimo.
Alisema mahindi huathirika katika hatua zake zote za ukuaji na
yaliyofikia kimo cha magoti (au urefu wa futi moja na nusu) majani yake
huathirika zaidi kwa kubadilika rangi kuwa ya njano, kukauka na baadaye
kuwa kahawia na kwamba dalili hizo huanzia kwenye shina la jani hadi
kwenye ncha ya jani changa pia mimea iliyosinyaa huonyesha dalili za
kukomaa kabla ya wakati.
Alisema kwa sasa wizara imekamilisha maandalizi ya sheria na kanuni za
kuzuia na kudhibiti ugonjwa huo na kwamba zitaanza kusambazwa ili kutoa
msukumo wa kisheria katika kukabiliana na athari za ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment