MSANII mahiri wa filamu hapa nchini, Wema Sepetu, amemnusuru
mwenzake Kajala Masanja, kwenda jela baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu kumhukumu kifungo cha miaka minane au faini ya sh milioni 13.
Kajala Masanja
Kajala alitiwa hatiani katika makosa ya kula njama kuhamisha umiliki
wa nyumba iliyokuwa imezuiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali isiuzwe.
Hukumu hiyo, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, ambapo
alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa Kajala na Faraja Chambo,
walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu yaliyofunguliwa mapema mwaka jana
mahakamani hapo.
Makosa hayo ni kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambapo washtakiwa wote kwa
pamoja, walitenda kosa hilo la kula njama la kuhamisha umiliki wa nyumba
iliyoko Kunduchi, Salasala, eneo ambalo halijapimwa jijini Dar es
Salaam.
Shtaka la pili ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 walihamisha isivyo
halali, umiliki wa nyumba hiyo, ambayo walikuwa wakiimiliki kwenda kwa
Emilian Rugalia, ambaye ndiye walimuuzia kinyume na kifungu cha
34(2)A(3), cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007 na shtaka la tatu ni la
kutakatisha fedha ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14, 2010, huku
wakijiua ni kinyume cha sheria.
Hakimu Fimbo alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili,
upande wa jamhuri umeweza kuithibitisha kesi hiyo na hivyo mahakama
hiyo imemtia hatiani Kajala katika kosa la kwanza na la pili tu, wakati
Chambo amepatikana na hatia katika makosa yote matatu.
Alisema, katika kosa la kwanza, Kajala na Chambo watatakiwa walipe
faini ya sh milioni tano kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu. Kosa la
pili watatakiwa walipe faini ya sh milioni nane au kwenda jela miaka
mitano kila mmoja.
Aidha katika kosa la tatu ambalo Chambo amekutwa na hatia peke yake,
atatakiwa alipe faini ya sh milioni 200 au kwenda jela miaka mitano na
kwamba adhabu hizo hazitakwenda pamoja. Hivyo Kajala peke yake
amehukumiwa kwenda jela miaka nane au kulipa jumla ya sh milioni 13.
“Mahakama imewakuta na hatia washtakiwa wote katika kosa la pili kwa
sababu ushahidi umethibitisha kuwa washtakiwa wote walikuwa wakifahamu
kuwa kulikuwa na hati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyokuwa imezuia
nyumba yao wasiiuze kwa sababu Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa
ilikuwa ikidai kuwa nyumba hiyo imepatikana kwa njia ya utakatishaji
fedha, lakini wao wakakaidi amri hiyo wakaamua kuiuza,” alisema Hakimu
Fimbo.
Akilichambua kosa la kwanza, alisema pia upande wa jamhuri umeweza
kulithibitisha kwa sababu kosa la pili limeweza kuthibitishwa.
Kuhusu shtaka la tatu, hakimu huyo alisema amemwachilia huru Kajala
kwa sababu upande wa jamhuri umeshindwa kuthitisha alishiriki vipi
katika upatikanaji wa fedha haramu, kwa sababu ilidaiwa kuwa Chambo
alizipata fedha haramu katika maelezo ya onyo kuwa alizipata fedha za
kujengea nyumba hiyo wakati akiwa mfanyakazi wa NBC.
“Na kwa mujibu wa maelezo ya onyo la Chambo, ambaye ni mume wa Kajala,
alikiri kuwa wakati akiwa mfanyakazi wa NBC, alikuwa akichukua fedha na
kuzituma kwa baadhi ya watu wa ofisi ya TTCL, watu ambao hawakuwa
wakistahili kulipwa na baada ya vyombo vya dola kuanza kumfuatilia,
akaamua kuiuza nyumba yake hiyo,” alisema Hakimu Fimbo.
Baada ya hukumu kutolewa, wasanii wa filamu nchini walikuwa wamefika
mahakamani hapo kufuatilia hukumu hiyo, walikusanyika katika viunga vya
mahakama hiyo na kuanza kujadiliana ili wachangishana fedha.
Lakini Wema, aliwataka wenzake wasichangishane, badala yake yeye
analipa sh milioni 13 na kuondoka katika eneo hilo na kisha kurejea
mahakamani hapo majira ya saa saba mchana na kulipa faini hiyo, kisha
kuondoka na Kajala, wakati Chambo akirudishwa gerezani kwa kushindwa
kulipa faini hiyo, pia anakabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji
fedha mahakamani hapo.
No comments:
Post a Comment