WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeingia kwenye kashfa
nzito ikidaiwa kuandaa semina hewa kwa walimu nchini, hivyo kuwaingiza
kwenye hasara ya gharama za usafiri na malazi.
Wakizungumza na gazeti hili kwa simu jana, baadhi ya walimu hao kutoka
mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, walidai kupata mwaliko wa barua
kutoka wizarani iliyoandikwa Februari 18, 2013.
Nakala ya barua hiyo yenye Kumb. Na. AHRD
/98/789/03S//40 iliyosainiwa na O.L. Michael kwa niaba ya Katibu Mkuu wa
wizara hiyo, ikiwa na kichwa cha habari kinachosomeka; Yah: Kuhudhuria
semina ya kitaifa ya rushwa, ukimwi, uzalendo na uwajibikaji kwa walimu
wa Tanzania Bara.
Walimu hao walidai kuwa mbali na barua hiyo pia walipigiwa simu
kupitia namba 0756-018031 kwa msisitizo, ikiwaomba kuhudhuria pasipo kukosa.
Barua hiyo inasema kuwa mara nyingine tena, Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi kwa ushirikiano mkubwa na Tanzania USAID, yaani taasisi ya
misaada ya watu wa Marekani kwa ajili ya maendeleo ya kimataifa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), zinafanya semina ya
kitaifa kwa walimu wa shule za msingi na sekondari wote kwa pamoja na
mada zinazowasilishwa hazihitaji mgawanyiko wowote.
Kwamba, semina hiyo itafanyika kuanzia tarehe 11 Machi hadi 26, mwaka
huu, katika Chuo cha Ualimu cha Kigurunyembe kilichopo mkoani Morogoro.
Barua hiyo ilisisitiza kuwa mara upatapo barua hii kwa ushirikiano na
mkuu wako wa shule, taratibu za ruhusa ya siku kumi na sita kutoka eneo
lako na kuja kwenye semina zianze kufanyika kuepuka kuchelewa.
“Watumishi wote waliochaguliwa kuhudhuria semina hii watapewa posho ya
kujikimu mara baada ya kufika na kufanya usajili, aidha kwa watumishi
ambao hawana uwezo wa kujisafirisha, shule au taasisi zinatakiwa
kuwasafirisha ili kufanikisha zoezi hili muhimu, ikiwa ni mpango wa
taifa,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Barua hiyo yenye muhuri wa wizara inaonesha kuwa nakala zake zilitumwa
pia kwa Kamishna wa Elimu, Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU na Mkurugenzi wa
USAID na kuaambatanishwa na ratiba.
Hata hivyo baadhi ya walimu waliotoka mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya na
Wilaya ya Mikumi mkoani Morogoro waliliambia gazeti hili kuwa baada ya
kufika Kigurunyembe na kumwona mkuu wa chuo, waliambiwa hakuna kitu kama
hicho na wala hana taarifa zozote za kufanyika kwa mkutano huo.
Kutwa nzima jana gazeti hili limejaribu bila mafanikio kuipigia namba
ya simu ambayo walimu walidai ilikuwa ikitumiwa kuwahamasisha. Hata
Waziri wa Elimu na naibu wake nao namba zao ziliita bila kupokewa.
No comments:
Post a Comment