JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni jijini Dar es Salaam
linawashikilia watu watano wakiwamo askari wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za mauaji ya dereva wa Bajaj, Yohana Cyprian
(20).
Watuhumiwa hao ambao majina yao hayakutajwa, wanadaiwa kumuua dereva
huyo Aprili 3, mwaka huu, saa 9:00 mchana huko Mbezi Beach kwa Mboma
jijini hapa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela aliwaeleza
waandishi wa habari jana kuwa kuuawa kwa Cyprian kuliamsha hasira kwa
baadhi ya wananchi.
Alisema kuwa wananchi hao walivamia Kituo cha Polisi Kawe kwa nia ya
kumchukua mtuhumiwa aliyedaiwa kuwapeleka wanajeshi hao waliosababisha
mauaji.
Kenyela aliongeza kuwa wananchi hao pia walizingira nyumba ya mmoja
wa askari mgambo wakitaka kuichoma kwa lengo la kumuua na kulipiza
kisasi.
“Baada ya kumuokoa mgambo huyo, wananchi walianza kuwarushia mawe na
marungu askari kisha kuchoma matairi barabarani ili wamchukue mtuhumiwa
na kumuua.
“Vurugu hizo zilidumu kwa saa mbili ndipo askari wakaamua kuwatawanya
kwa mabomu ya machozi na risasi za baridi wananchi waliokuwa wanafanya
vurugu,” alisema.
Kenyela aliwataja askari waliojeruhiwa kuwa ni E1739 D/CPL Alson,
D.9054 DCPL Felix na G.5407 PC Azizi aliyepigwa na jiwe kichwani.
Alifafanua kuwa katika vurugu hizo watu 12 walikamatwa na wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
No comments:
Post a Comment