HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kutotekeleza ahadi zake alizozitoa
wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2010, imeanza kuwatia hofu baadhi ya
wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa huenda wasichaguliwe tena
kurudi bungeni.
Hofu hiyo ilijidhihirisha bungeni jana wakati Mbunge wa Mwibara,
Kangi Lugora (CCM) alipouliza swali la nyongeza na kutaka kujua ni
kwanini serikali haipeleki orodha zote za ahadi zilizoahidiwa na Rais
Kikwete wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu 2010 ili wabunge waweze
kujadili sehemu muhimu ya kuanza kwa utekelezaji huo.
“Kutokana na ahadi za rais kutokutekelezwa, kuna uwezekano mkubwa
wabunge wote wasirudi bungeni hapa kwani wabunge ndiyo wanaosakamwa na
wapiga kura wao ikifika kipindi cha uchaguzi.
“Wapiga kura watatuuliza ni kwanini ahadi hizo hazijatekelezwa na
wakati huo rais hataweza kuwajibika japo yeye ndiye aliyetoa ahadi
hizo,” alisema Lugora na kuhoji ni kwanini serikali isilete orodha ya
ahadi zote zilizoahidiwa na rais.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk. Cyril
Chami (CCM) alitaka kujua ni lini serikali itatekeleza ahadi ya kujenga
kwa kiwango cha lami barabara ya Old Moshi inayoanzia Kiboriloni
kupitia Kikarara, Tsuduni hadi Kadia.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri alikiri
kuwa katika kipindi cha kampeni za uchaguzi 2010, rais alifika katika
maeneo mbalimbali na kutoa ahadi.
Alisema ahadi zote ambazo alizitoa zitatekelezwa kulingana na hali ya kifedha inavyoruhusu kwani ahadi ya rais ni agizo.
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA) alihoji ni kwanini serikali
haina mipango maalumu ya kuhudumia barabara ambazo zipo milimani ikiwa
ni katika utekelezaji wa ahadi ya rais.
Akijibu swali hilo, Mwanri alisema atakaa na mbunge huyo ili
kuhakikisha wanaangalia ni jinsi gani ya kuweza kuweka mipango maalumu
ya ujenzi wa barabara hizo ili kuwapa wepesi watumiaji ikiwa ni pamoja
na kupunguza ajali.VIA Tanzania daima
No comments:
Post a Comment