MKURUGENZI wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday
Kayuni, amewasihi wachezaji wa soka nchini kutotumia dawa za kulevya
kama bangi ikiwa wanataka kupata mafanikio ya kweli katika mchezo huo.
Mbali ya bangi, Kayuni amewasihi wachezaji wenye malengo ya kufika
mbali katika mchezo huo kuachana na imani za kishirikina kwani vitu
hivyo havina nafasi katika soka.
Kayuni ambaye ni kocha wa soka kitaaluma aliyewahi kufundisha timu
mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, aliyasema hayo jana katika semina
ya siku moja ya wachezaji na viongozi wa klabu sita za Mkoa wa Dar es
Salaam zinazoshiriki Ligi Daraja la Pili ngazi ya kanda iliyoanza jana
hadi Aprili 31.
Kayuni alisema imani potofu za ushirikina na matumizi ya bangi ni
hatari inayoikabili soka ya Tanzania na kuwataka wachezaji wa timu hizo
na nyingine nchini kuyaepuka hayo yanayowavunjia heshima mbele ya
jamii.
“Ninawaomba viongozi mtambue majukumu yenu na kuepuka kufanya au
kuingilia mambo yasiyo wahusu, kwani kama mtaheshimiana hali inaweza
kuwa nzuri katika soka, hususan ndani ya Mkoa wenu wa Dar es Salaam,
pia wachezaji muwe na nidhanmu nzuri ili muweze kufanikiwa katika
malengo yenu kiuchezaji,” alisema Kayuni aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa
Chama cha Makocha wa Soka (Tafca).
Akizungumzia semina hiyo, Katibu Mkuu wa DRFA, Msanifu Kondo, alisema
inalenga kuwaongezea uelewa viongozi wa timu kwa maana ya manahodha na
viongozi wa klabu katika kukuza ufanisi wa utendaji kazi katika
kuendeleza soka kwenye mkoa huo.
Timu zinazoshiriki hatua ya sita bora iliyoanza jana ni Boom FC,
Friends Rangers, Abajalo FC, Red Coast, Dar Break na Shariff Stars
ambazo zitakuwa zikitumia viwanja vya Sekondari ya Benjamin Mkapa,
Kinesi na Makulumla.
No comments:
Post a Comment