SHILINGI milioni 143 zimetengwa kwa ajili ya kazi ya kufunga
umeme wa gridi ya taifa kwenye hospitali ya AIC Mkula iliyopo Wilaya
mpya ya Busega mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene aliliambia
Bunge jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Busega, Dk. Titus
Kamani (CCM).
Kamani alitaka kujua lini serikali itafunga umeme wa gridi katika hospitali hiyo.
Pia alitaka kujua tatizo gani limekwamisha utekelezaji wa mpango huo kwa muda mrefu sasa.
Akiendelea kujibu swali hilo, Simbachawene alisema kazi ya kufunga
umeme wa gridi kwenye hospitali hiyo imejumuishwa katika mpango kabambe
wa umeme vijijini awamu ya pili chini ya Wakala wa Nishati Vijijini
(REA).
Alisema fedha hizo zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa njia ya umeme
msongo wa kilovoti 33 urefu wa kilomita 2, njia ya umeme msongo wa
kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 3, ufungaji wa transfoma moja ya kVA 200
na kuunganishia umeme wateja zaidi ya 50.
“Zabuni ya kuwapata wakandarasi ilitangazwa Desemba 2012 na
kufunguliwa Machi, mwaka huu… kazi za ujenzi zinatarajiwa kuanza wakati
wowote ndani ya mwaka huu,” alisema.
No comments:
Post a Comment