KAULI ya Mbunge wa Uzini, Mohammed Seif Khatib (CCM) kwamba
wabunge wa viti maalumu CHADEMA wamepata nafasi hizo kwa vile ni wake,
wapenzi na wachumba wa viongozi wa chama taifa, imesababisha wabunge hao
kuvamia ofisi ya Spika kushitaki, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Wabunge hao pia walilalamika kauli ya udhalilishaji iliyotolewa hivi
karibuni bungeni na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) kwamba
baadhi ya wabunge wanapata mimba zisizotarajiwa.
Khatib alitoa kauli hiyo ya udhalilishaji mjini Morogoro katika
mkutano wa hadhara wa CCM uliowashirikisha viongozi wa kitaifa akiwemo
Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana.
Habari zilisema kuwa wabunge hao
walifika katika Ofisi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda juzi na
kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya kauli ya Khatib.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa wabunge
hao walishangazwa na kauli ya Khatib ambaye hivi karibuni amechaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa Bunge, kusaidia shughuli za Bunge pale spika au naibu
wake wanapokuwa hawapo.
“Hii kauli ni mwendelezo wa vitendo vya udhalilishaji kwa wabunge
wanawake vinavyofanywa na wabunge wanaume, na kibaya zaidi kauli hiyo
safari hii imetolewa na Mwenyekiti wa Bunge,” alisema mmoja wa wabunge
hao waliokwenda kwa spika.
Walimtaka Khatib awaombe radhi vinginevyo watachukua hatua zaidi kupinga udhalilishaji huo.
Akijibu malalamiko ya wabunge hao, Makinda aliungana nao kwa kusema
kauli za Khatib na Lusinde hazipaswi kufumbiwa macho kwani ni dhahiri
zimewadhalilisha wabunge wanawake.
“Kwa wanawake wenye hadhi ya ubunge, huwezi kusema wanapata mimba za bila kutarajia na hii isiwafanye muone aibu kuzaa.
“Hata kama hujaolewa huna sababu ya kuona aibu kwamba utaambiwa umepata mimba ya bila kutarajia,” alisema.
Katika hatua nyingine, Makinda alisema serikali inakamilisha ujenzi wa
jengo moja ndani ya eneo la Bunge ambalo litakuwa kwa ajili ya wabunge
wajawazito na wenye watoto wachanga.
Kwa mujibu wa Spika Makinda, mbunge mwenye mtoto mchanga ataruhusiwa
kuja na wasichana wa kazi ambaye atakaa kwenye jengo hilo wakati vikao
vya Bunge vikiendelea.
“Kwa hiyo kama unataka kunyonyesha mtoto, unatoka ukumbini, unaingia
kwenye jengo hilo unanyonyesha, ukimaliza unarudi bungeni kuendelea na
kazi,” alisema.
Katika mkutano huo wa CCM, ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha
Televisheni ya Taifa, Khatib ambaye pia ni Katibu wa Oganaizesheni ya
chama hicho, alisema CHADEMA ina wabunge wa kuchaguliwa na viti maalumu.
Alifafanua kuwa ukiacha wale wa kuchaguliwa, wabunge wa viti maalumu
walipatikana kutokana na kuwa wachumba, wake na wapenzi wa viongozi wa
CHADEMA Taifa.
Khatib huku akifahamu wazi kuwa wabunge hao wamepatikana kwa utaratibu
wa kikatiba ambao umeidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
aliongeza kuwa CHADEMA inaongozwa na wazinzi wenye dhambi wasiofaa
kwenda Ikulu.
Hivi karibuni baada ya baadhi ya wabunge wa CCM akiwemo Lusinde kuibua
matusi kwa wanawake, Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM)
aliwataka wabunge wanawake kwa niaba ya wanawake wengine wakatae vitendo
hivyo.
Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wabunge Wanawake (Ulingo)
pia alielezwa kukerwa na mifano ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi (CHADEMA) aliyenukuu maandiko ya Biblia Takatifu, yasemayo
“mwanamke mpumbafu huivunja ndoa yake mwenyewe”.
No comments:
Post a Comment