Baada ya Tanzania kutajwa kuwa nchi ya pili kwa umaskini kwenye
ukanda wa Afrika Mashariki, wachumi wamesema hali hiyo inachangiwa na
Serikali kutokuwa na mipango thabiti ya kuwasaidia wakulima na kuinua
sekta ya viwanda nchini.
Wakitoa maoni yao kwa njia ya simu jana walisema takribani asilimia 80 ya Watanzania ni maskini wanategemea kilimo kuendesha maisha yao, hivyo ili kuwainua ni vyema Serikali ikatenga bajeti kubwa katika sekta hiyo pamoja na kuweka miundombinu ya kilimo ya kutosha.
Utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), unaonyesha kuwa Burundi ndiyo nchi inayoongoza kwa kuwa na watu wengi maskini ikifuatiwa na Tanzania kwenye eneo hilo.
Burundi inaongoza kwa kuwa na asilimia 81.32, Tanzania ikifuatia na asilimia 67.87, Rwanda asilimia 63.17, Kenya asilimia 43.37 na Uganda 38.01. Utafiti huo ulijikita zaidi katika kuangalia idadi ya watu wanaoishi kwa dola 1.25 kwa siku.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) alisema umaskini wa Watanzania unachangiwa na mengi ikiwa ni pamoja na kuja na mpango wa Kilimo Kwanza bila kuboresha miundombinu ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji.
Alisema kuzorota kwa sekta ya kilimo kunachangiwa na kuduma kwa sekta ya viwanda na kwamba Kenya na Uganda wamepiga hatua kwa sababu ya kuwekeza zaidi katika viwanda.
Kiongozi wa Chuo cha Uongozi na Ujasiriamali, Dk Donath Olomi alisema umaskini wa Watanzania unachangiwa na Serikali kutokuwa na mipango endelevu, kushindwa kusimamia miradi yake pamoja na kutofuata sheria zilizopo.
Alisema Serikali inatakiwa kuweka miundombinu ya umwagiliaji na kuachana na kilimo cha kutegema mvua na kutenga maeneo maalumu ya kilimo.
No comments:
Post a Comment