Liwale balaa
Wananchi wasiojulikana
wamechoma moto ofisi na nyumba za mbunge wa Liwale mkoani Lindi, Faith
Mitambo pamoja na nyumba za viongozi wa CCM na wa vyama vya ushirika
vya msingi kwenye mji wa Liwale.
Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi likianzia katika Kijiji cha
Liwale B ambako wakulima wa Chama cha Msingi cha Minali walikataa
malipo ya korosho ya sh 200 kwa kilo yakiwa ya pili badala ya sh 600
waliyoahidiwa mwaka jana.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, vurugu
hizo zilitokea saa tisa alasiri, huko wilayani Liwale ambapo kundi la
watu wanaodhaniwa kuwa wakulima wa korosho walijaribu kuzuia gari
lililokuwa na malipo.
Alisema kuwa wakulima hao walikuwa wakipinga malipo ya pili ya
korosho na hivyo kuanza kufanya vurugu na uharibifu mkubwa wa mali.
Senso alisema hadi jana taarifa za awali zilionesha kuwa nyumba 14
zilichomwa moto, baadhi ya mifugo ilijeruhiwa na kuangamizwa na
kufanyika uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Alisema kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said
Mwema alituma timu maalumu ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai nchini (DCP), Issaya Mngulu kwenda kuongeza nguvu
kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa hali ya amani na utulivu inarejea haraka
na wale wote waliohusika kufanya vitendo vya uhalifu wanakamatwa na
kufikishwa mahakamani ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hadi sasa
watuhumiwa 19 wamekamatwa kwa mahojiano,” alisema.
Wakati taarifa za polisi zikieleza hivyo, mashuhuda wa tukio hilo
walisema kuwa Mwenyekiti wa chama hicho cha ushirika, Mohamed
Limbwilindi alikwenda kijijini hapo akiwa na sh milioni 61.4 ambazo
wakulima hao wangelipwa sh 200 kwa kila kilo ya korosho.
Kwamba wengine ambao hawakupewa malipo ya awali walielezwa kuwa
watalipwa sh 800, jambo ambalo lilizua mtafaruku miongoni mwao na hivyo
kurudisha fedha.
Kutokana na hali hiyo, ilielezwa kuwa wananchi wenye hasira walianza
kukateketeza moto ofisi ya chama hicho na nyumba ya mwenyekiti kisha
pia nyumba ya katibu wake, Juma Majivuno.
Baada ya vurugu hizo huko Liwale B, alasiri vurugu hizo zilihamia mjini Liwale ambako uharibifu mkubwa wa mali ulifanyika.
Wananchi hao walichoma ofisi ya mbunge, duka la pembejeo la Hassan
Mpako, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja mjini
Liwale pamoja na nyumba yake.
Akizungumzia tukio hilo, Mpako alisema; “niliona kundi kubwa la watu
wanakuja nyumbani kwangu saa 3 usiku wakiwa wamebeba nondo, mawe pamoja
na madumu ambayo nadhani yalikuwa na petroli,” alisema.
Mpako alifafanua kuwa watu hao walimweleza; “tunataka fedha zetu za
korosho” mazingira aliyodai kuwa yalimlazimisha atimue mbio ili
kujisalimisha.
Alisema watu hao waliteketeza nyumba yake pamoja na trekta dogo la
mkono, pikipiki, jenereta pamoja akiba ya pembejeo za kilimo ambazo
zilikuwa dukani.
Wengine waliochomewa nyumba ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mohamed Ngomambo ambaye alisema anamwachia Mungu.
“Kama nimepoteza wazazi ambao wana thamani kubwa maishani mwangu nyumba ni kitu gani?” alisema Ngomambo.
Kutokana na vurugu hizo, kundi kubwa la askari wa kutuliza ghasia
(FFU) toka Lindi limewasili wilayani Liwale kudhibiti hali ya usalama
ambayo imetoweka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alizungumza kwa
simu akisema kuwa mbunge wa Liwale nyumba zake mbili na ofisi vilichomwa
moto.
Pia Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Chande nyumba yake moja ilichomwa moto
huku mwenyekiti wa Halmashauri ya Liwale, Abasi Matulilo naye nyumba
yake ilichomwa.
“Meneja wa Chama cha Msingi cha Ilulu, Hamza Mkungura nyumba zake
mbili ziliteketezwa na duka la dawa na pembejeo vile vile yaliteketezwa
huku mifugo ikijeruhiwa na kuchinjwa,” alisema.
Kamanda aliwataja wengine walioathirika na vurugu hizo kuwa ni meneja
mikopo wa NMB, Mohamedi Pimbi ambaye duka lake la vifaa vya umeme
lilichomwa pamoja na duka la Kanisa Katoliki.
Aliwataja pia Diwani wa CCM, Hasan Muyao na Diwani wa Viti Maalumu
Amina Mnocha kuwa nyumba zao zilichomwa pamoja na nyumba ya mjumbe wa
NEC wa chama hicho, Hemedi Ngonani ambaye aliharibiwa maduka ya simu na
vyakula.
No comments:
Post a Comment