BIASHARA ya damu imebainika kuwapo wilayani Bunda mkoani Mara.
Damu ‘uniti’ moja inauzwa kati ya sh 15,000 hadi sh 20,000 kisha
kuwaongezea wagonjwa wenye upungufu wa damu hususan watoto na
wajawazito.
Biashara hiyo imebainika hivi karibuni na kushika kasi katika Kata ya Nyamuswa, Tarafa ya Ikizu wilayani Bunda mkoani Mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wateja wa damu hiyo ambao ni
wagonjwa wanaotibiwa katika Kituo cha Afya cha Ikizu, wanasema kuwa
biashara hiyo ina mikono ya madaktari na wauguzi wa kituo hicho.
Wanasema mgonjwa anayekwenda katika kituo hicho na kugundulika kuwa
ana upungufu wa damu hasa watoto na wajawazito huambiwa kuwa watoe damu
au wanawaitia vijana wanaokuwa nje ya uzio wa hospitali hiyo na
kufanya makubaliano na ndugu wa wagonjwa.
“Wakiwaita vijana hao ili kutoa damu, wanataka kupewa sh 20,000 na
mkiwabembeleza wanashusha hadi sh 15,000,’’ anasema mgonjwa Angela
Hamisi.
Mganga Mkuu Kiongozi wa kituo hicho cha afya cha Ikizu, Dk. Abahehe
Kanora, anasema malalamiko hayo si ya kweli bali uongozi wa kituo
ulikubaliana na kamati ya afya ya eneo hilo kuwa kutokana na uhaba wa
vitendanishi ikiwemo vifaa na dawa za kupimia damu kila anayeongezewa
damu anachangia sh 2,000.
“Malalamiko hayo si kweli bali kumekuwa na tabia kwa baadhi ya
wagonjwa na ndugu zao wanaohitaji damu wakiambiwa kuwa hatuna damu
ndipo wanalazimika kuwatafuta watu nje ya kituo na kuja nao ili
kuwatolea damu hao, labda ndio wanaowauzia lakini sisi hapa anayechangia
damu na anayeongezewa kila mmoja hutozwa sh 2,000,’’ anasema Dk.
Kanora.
Anafafanua kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuchangia gharama ya vifaa
na dawa za kupimia kundi la damu zao na kwa siku moja kituo hicho cha
afya kinatumia ‘uniti’ 10 za damu na nyingi hutumika kwa watoto chini
ya umri wa miaka mitano.
Anapoulizwa kuwa kama anajua kuwa hata kuchangisha fedha kwa wagonjwa
hao na wanaochangia damu ni kosa kutokana na sera ya afya ya mwaka
2007 katika kipengele cha damu salama, anasema kuwa analijua hilo
lakini kutokana na ukosefu wa vitendea kazi na damu yenyewe kutoka
katika Benki ya Damu Salama ya Kanda iliyopo Bugando mkoani Mwanza
ndiyo maana wanalazimika kufanya hivyo.
“Unajua tunalazimika kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya watu, maana
upatikanaji wa damu ni mgumu sana na hata tukisema kuwa watu wachangie
damu ni wachache wanaojitokeza na mkipeleka mkoani ili kupeleka Mwanza
tutapoteza maisha ya watu wengi sana,’’ anasema Dk. Kanora.
Anasema kutokana na ukosefu wa damu salama katika kituo hicho cha
afya watoto wengi hupoteza maisha baada ya kuumwa kwa muda mrefu
ugonjwa wa malaria huku wakicheleweshwa kufikishwa hospitalini na wengi
wao wanatoka Serengeti.
Kabla ya kukutana na Dk. Kanora nilikutana na Dk. Safari Matundwe
aliyekuwepo hospitalini hapo lakini hakuweza kutoa msaada wowote kwa
mjamzito, Furaha Nyateli, mkazi wa Sarama Kati aliyekuwa akihitaji
msaada wa kujifungua ndani ya wodi ya wajawazito.
Akizungumza kwa uchungu na kusema hali hiyo ndivyo ilivyo katika
kituo hicho, binti aliyeongozana na mjamzito huyo, Doi Hamis, anasema
kuwa chupa ya uzazi ya mwenzake ilikuwa imepasuka tangu saa nne asubuhi
lakini hakupewa msaada wowote licha ya kulazwa mpaka majira ya saa tisa
baada ya waandishi kufika na kujionea hali ya mjamzito huyo na kuamua
kuhoji kulikoni.
Akielezea hali hiyo, Dk. Safari anasema hali hiyo inatokana na
uchache wa watumishi hasa wakunga, ambapo siku hiyo alikuwepo muuguzi
mmoja tu aliyekuwa akihudumia wagonjwa wa aina zote katika wodi nne
zilizopo katika kituo hicho cha afya.
Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda, Adelaida Masige,
anasema kuwa katika wilaya hiyo kumekuwa na tatizo kubwa la damu salama
ingawa mwanzo walikuwa wakijitolea zaidi wafungwa na wanafunzi.
“Damu salama ni tatizo kubwa, kinachofanyika wagonjwa wanaotaka
kuongezewa damu wanakuja na ndugu zao, tukiwachukua damu tunapima
Virusi Vya Ukimwi (VVU) na magonjwa ya zinaa, lakini hakuna utafiti
uliofanyika kujua kama walioongezewa damu wameambukizwa au la,’’
anasema Adelaida.
Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH ),
Revocatus Kato, anasema kwa upande wa hospitali hiyo damu ni tatizo
kubwa na wagonjwa wanaofika hapo wanalazimika kuchangia gharama za
mifuko ya kuwekea damu.
“Tunawataka wagonjwa au ndugu zao kutoa sh 2,500 kwa ajili ya
kununulia mifuko ya kukusanyia damu, mirija ya dripu ya kumwingizia
mgonjwa sh 2,000 na kama atakuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji anatoa
pesa ya nyuzi sh 5,000 na kumshona ni sh 8,000,’’ anasema kaimu muuguzi
huyo.
Lakini mjamzito, Agness Baraka, mkazi wa Kijiji cha Kambubu, Kata ya
Nyamang’uta, anasema aliwahi kukimbizwa katika Hospitali ya DDH akiwa
mjamzito ambapo alilipa sh 16,000 kwa ajili ya nyuzi za kumshonea tu
baada ya kufanyiwa upasuaji mbali na gharama za damu.
Diwani ya Kata ya Nyamang’uta, Kalemba Jonathan Ilubi, anasema kuwa
ni kweli kuna ongezeko kubwa la vifo vya watoto chini ya miaka mitano
kutokana na kupungukiwa damu na kucheleweshwa kupelekwa hospitali lakini
wananchi wengi wanadai kuwa wanaogopa kuwapeleka hospitali watoto wao
ili kukwepa (kauli mbaya) kutukanwa na wahudumu wa vituo vya afya.
Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto wilayani humo,
Daines Lyimo, anasema sababu nyingine inayochangia kupungua kwa damu
kwa wajawazito ni kutokana na kukosa lishe ya kutosha.
“Lishe kwa sasa katika wilaya hii hasa kwa wajawazito ni tatizo,
ambapo hata samaki hawapatikani kwa wingi kama zamani, minofu yake
inapelekwa viwandani na wanawake wakila samaki minofu inaongeza madini
ya chuma na damu mwilini,’’ anasema Daines.
Anasema kwa sasa wajawazito kumi wanaofika kujifungua katika vituo
vya afya au hospitalini, kati yao wawili hugundulika kuwa na upungufu
wa damu na kutakiwa kuongezewa damu.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Rainer Kapinga, anakiri kuwa kuna
tatizo la upatikanaji wa damu salama wilayani humo na anazo taarifa za
baadhi ya watumishi kuhusika kuuza damu kwa wagonjwa na tayari
watumishi watatu wamewajibishwa kutokana na kushirki kuuza damu.
“Utaratibu wa halmashauri tunanunua vifaa vyote vya kutolea damu na
kuwekea lakini binadamu wana mambo yao, hasa watu wa maabara na tayari
watu watatu wamewajibishwa kutokana na suala hilo,’’ anasema Dk.
Kapinga.
Anasema ukubwa wa tatizo hilo la upungufu wa damu wilayani humo kuwa
asilimia 60 ya wajawazito hupungukiwa damu kutokana na ukanda huo kuwa
ni ukanda wa malaria.
“Asilimia 60 ya wajawazito hupungukiwa damu kutokana na ukanda huu
kuwa wa malaria na mtu anapokuwa mjamzito kinga zake hupungua,’’
anasema Dk. Kapinga.
Katika Wilaya mpya ya Butiama mkoani Mara, nako tatizo la damu ni
kubwa ambapo Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Butiama, Dk. Joseph
Musagafa, anasema vifo vingi hasa vya watoto chini ya miaka mitano
wanakufa kutokana na ukosefu wa damu.
Anasema hospitali hiyo wamejipanga kutoka na kwenda kuzungumza na
jamii kuhusu umuhimu wa kuwawahisha wajawazito na watoto hospitalini
wanapoona wanaumwa.
“Vifo vingi vya watoto chini ya miaka mitano vinatokea kwa kukosa
damu na kuwachelewesha kufika nao hospitali,’’ anasema Dk. Musagafa.
Anasema sababu nyingine zinazosababisha mpaka hali hiyo ya ukosefu
wa damu hasa kwa watoto chini ya miaka mitano kuwa ni pamoja na baadhi
ya wazazi wakiona watoto wao wanaumwa wanawanunulia dawa kwenye maduka
ya dawa muhimu za binadamu, wengine huamini kuwa watoto wao wamerongwa,
hivyo kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji.
“Wengine wanapenda kuwaleta watoto wao mapema lakini wanakosa usafiri
wa kuwafikisha mapema na baadhi hawana uchumi mzuri wa kuwawezesha
kufika hospitali na kumudu gharama,’’ anasema Dk. Musagafa.
Kwa upande wa wanawake anasema kuwa wengi wao wanajifungulia
majumbani kutokana na sababu mbalimbali kama alizozitaja hapo juu,
ikiwamo sababu ya usafiri na miundombinu huku akitolea mfano maeneo ya
Bugoji, Majile na Mulangi, ambayo yapo umbali wa kilometa 100 ili
kufikia hospitali hiyo.
Kuhusu uuzwaji wa damu anasema hawana damu kabisa hivyo wanalazimika
kuchukua kwa ndugu wa wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo na baada
ya kuchukua damu hiyo wanapima VVU na kaswende kisha kumuongezea
mgonjwa.
Anakiri kuwa kuhusu ubora wa damu hiyo wanakuwa hawana uhakika zaidi
bali wanachoangalia ni kuokoa maisha ya mgonjwa ambaye huchangia sh
3,000 kwa ajili ya chupa ya kutunzia ambapo anasema wanalazimika
kuwatoza wagonjwa au ndugu zao fedha hiyo ili kuchangia gharama ya
vifaa hivyo.
“Tunatoza fedha hiyo ili kununulia begi za kuhifadhia damu hiyo na
hali hii tunalazimika kutokana na kutovipata kutoka Bohari ya Dawa
(MSD),’’ anasema mganga huyo huku akiwaambia wauguzi wamtundikie haraka
damu, Remmy Wambura, mama aliyefika hospitalini hapo baada ya
kujifungua salama nyumbani uzao wake wa saba na kupoteza damu nyingi.
Hospitali ya Butiama ndiyo inayotibu hata familia ya hayati Mwalimu
Julius Nyerere, ambapo Dk. Peter Mwera anasema kila siku ya Alhamisi
endapo Mama Maria Nyerere akiwapo kijijini hapo wanakwenda kumfanyia
uchunguzi wa afya yake.
Dk. Mwera anasema ni zaidi ya awamu mbili amekwenda kumfanyia
uchunguzi wa afya Mama Maria Nyerere na kwamba kuna awamu aliwaambia
kuwa anawachosha hivyo atalazimika yeye mwenyewe kwenda katika
hospitali hiyo ili kufanya uchunguzi wa afya yake lakini bado hajafanya
hivyo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara, Dk. Iragi
Ngerageza, anasema tatizo la damu salama ni kubwa katika hospitali hiyo
ambapo wanalazimika kukusanya damu kutoka kwa wagonjwa.
Anasema ili kupata vipimo wanapeleka mkoani Mwanza ambako ndiko kuna
vipimo sahihi vya kuthibitisha kuwa damu hiyo ni salama au iharibiwe
ambapo kwa Hospitali ya Mkoa wa Mara hutumia sh 120,000 kwa ajili ya
kulipa kwenye basi kupeleka damu hiyo na watumishi wanaopeleka na
kurudi na damu, na kwa wiki anasema damu inapelekwa mara nne.
Wanalazimika kusafirisha damu hiyo kwa kutumia mabasi ili kupunguza
gharama, ambapo anasema kuwa wakitumia gari la serikali linatumia lita
90 za mafuta kwenda tu na wanalazimika kuwalipa dereva na mhudumu wa
afya anayepaswa kukabidhi damu hiyo katika benki ya damu, hivyo
wanapunguza matumizi hayo kwa kusafirisha kwa mabasi ya abiria na
kumlipa mtumishi mmoja tu.
Anasema matumizi ya damu ni makubwa, ambapo watoto chini ya miaka
mitano, majeruhi na wajawazito kwa siku wanatumia zaidi ya ‘uniti’ 8
mpaka 10.
Hata hivyo, licha ya kuwapo kwa upungufu huo wa damu unaosababisha
vifo vingi vya wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano,
imeelezwa kwamba baadhi wanakufa kutokana na imani za dini zao
zinazokataza kuongezewa damu, kwa madai kuwa ni sawa na kuchukua kiungo
cha binadamu mwingine.
Habari hii na Gordon Kalulunga wa Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment