JESHI Polisi Mkoa wa Katavi linawashikilia wanafunzi watano wa
Shule ya Sekondari ya Mizengo Pinda iliyopo Kata ya Kibaoni Wilaya ya
Mlele kwa tuhuma za kuwaongoza wanafunzi wenzao kufanya vurugu.
Katika vurugu hizo, wanafunzi hao wanadaiwa kuharibu majengo ya
shule na kisha kumjeruhi mwalimu wao wakimtuhumu yeye na mkuu wa shule
hiyo kuwa walimloga mwanafunzi mwenzao akawa na ugonjwa wa mapepo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Emanuel Nley aliwataja
wanafunzi waliokamatwa kuwa ni Isaya Benezeti (18),Aloyce Nshaki
(17),Coaster Petro (19), John Salumu (19) na January Sanane (20) wote
wa kidato cha nne.
Alisema kuwa siku ya tukio Aprili 21, mwaka huu, saa 2:30 usiku,
watuhumiwa hao waliwaongoza wanafunzi wenzao kuharibu jengo la utawala
kwa mawe na matofali kisha kuvunja mlango na madirisha.
Nley aliongeza kuwa baada ya kuharibu jengo hilo, wanafunzi
walikwenda nyumbani kwa mkuu wa wa shule, Alko Kaminyoge, wakimtuhumu
pamoja na mwalimu wa taaluma, Boniface Salamba, kujihusisha na
ushirikina.
Aliongeza kuwa baada ya hapo walivamia nyumba ya Mwalimu Boniface na
kufanya vurugu kisha walimshambulia kwa mawe na kumsababishia maumivu
sehemu mbalimbali za mwili.
Kamanda alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
No comments:
Post a Comment