BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limedaiwa kumtelekeza
mbunge wa Viti Maalumu, Christina Mughwai (CHADEMA), kutoka mkoa wa
Singida.
Mughwai ambaye amelazwa tangu Aprili 14, mwaka huu, katika Hospitali
ya Agha Khan, jijini Dar es Salaam, jana alilazimika kurejeshwa
nyumbani kwake ili aendelee kusubiri safari ya kupelekwa nje ya nchi kwa
matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wanafamilia, hali ya mbunge
huyo si nzuri kwani pamoja na kulazwa Aga Khan, alishauriwa na madaktari
kwenda India kwa matibabu zaidi ila Bunge limechelewesha safari hiyo
kwa siku kumi tangu ushauri huo ulipotolewa.
Akizungumza na gazeti hili jana, mdogo wa mbunge huyo, Tundu Lissu, alisema dada yake alitoka hospitalini jana mchana.
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), alisema
kuwa madaktari walimweleza mgonjwa wao kuwa hana sababu ya kuendelea
kubakia hospitalini akisubiri safari ya India.
“Walimshauri akasubirie nyumbani, ingawa hali yake sio nzuri,” alisema Lissu.
Alipoulizwa kama taratibu za kumpeleka India zimefanyika au la,
Lissu alisema zilipaswa kuwa za kibunge lakini wamecheleweshwa sana na
sasa wanataka kuchukua jukumu hilo kama familia ili impeleke akapate
matibabu.
Lissu aliongeza kuwa alipowasiliana na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas
Kashililah, ili kujua msimamo wa ofisi yake, tangu juzi alikuwa
akiahidiwa kuwa angempigia kumweleza utaratibu, lakini hadi jana alikuwa
hajapigiwa.
Alipoulizwa kama kuna utaratibu wa kumsafirisha kumpeleka India kwa
matibabu zaidi, Dk. Kashilillah alisema; “Mbona unaniuliza hivyo kwani
wewe umeshajua ugonjwa anaoumwa hadi uniulize hivyo? Sisi tunafuata
ushauri wa madaktari, wakisema tumpeleke tutafanya vile, wao ndio
wanaamua.”
No comments:
Post a Comment