NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' amewahurumia Simba na
kudai kuwa wao Jangwani wana sababu kubwa mbili zitakazowapa ushindi
mbele ya Simba na huu ndio muda wao wa kulipa kisasi.
Yanga na Simba zinakutana Jumamosi katika pambano la Ligi Kuu Bara huku Simba wakitaka ushindi kulinda heshima na kujihakikishia nafasi ya tatu wakati Yanga wanataka kulipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 msimu uliopita.
Cannavaro aliliambia Mwanaspoti kuwa kikosi chao kipo fiti bila presha, wanasubiri siku hiyo waingie uwanjani na kuwaonyesha Simba soka la maana.
Tayari Yanga imepiga kambi Pemba na Simba imetulia Unguja.
"Tuna sababu kubwa mbili za kuifunga Simba; kwanza tayari sisi ni mabingwa hivyo tutaingia uwanjani bila presha na pili fedha tulizoahidiwa ni nyingi hivyo hatuwezi kuacha zipotee, tunaomba Mungu siku hiyo wachezaji wote wawe wazima, tuwaonyeshe Simba soka linavyochezwa na kuonyesha kila mmoja kuwa hatukuchua ubingwa kwa kubahatisha,"alisema.
Cannavaro alisema hawezi kuidharau Simba eti kwa
sababu ina wachezaji wengi vijana wa kikosi B bali wataingia uwanjani
kupambana na Simba kama ya siku zote.
"Wale ni vijana lakini wanacheza vizuri, wamepambana na timu nyingi za Ligi Kuu hivyo mechi itakuwa ngumu na tutakabiliana nao kama siku zote na hatuwezi kuwadharau ingawa kuwafunga kuko pale pale," alisema Cannavaro ambaye ni miongoni mwa mabeki wa Ligi Kuu waliocheza mechi nyingi za timu ya Taifa Stars na Zanzibar Heroes.
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu
Simba na Yanga zilitoka sare ya bao 1-1, mabao yakifungwa na Amri Kiemba
wa Simba na Yanga wakasawazisha kupitia kwa Said Bahanuzi ambaye
hakuonyesha cheche zake kama ilivyotarajiwa msimu huu.
No comments:
Post a Comment