KIUNGO wa mabingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Haruna
Niyonzima 'Fabregas' amewashangaa Yanga kwa kukubali visingizio vya
Simba kwamba inatumia wachezaji yosso na amewaambia kuwa wasikubali
kuzugwa.
Haruna ametamka kwamba wao wachezaji wa Yanga walioko kambini Zanzibar wanajua wanakumbana na Simba kamili kwavile wanawajua vilivyo kiumri wachezaji wa Simba 'wanaolazimishwa' kuitwa yosso.
Kiraka huyo anasema kwamba tofauti ya kikosi cha Yanga na kile cha Simba ni maumbo ya wachezaji na uzoefu tu wala si kweli kwamba ni wadogo na hata kama ni wadogo ndio walioaminika kwa kocha kuliko wakongwe waliosimamishwa.
Alisema mara nyingi mtoto si mchezaji na kama wao (Simba) wana wachezaji watoto, basi wangebaki nyumbani na wazazi wao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisingewaruhusu kucheza soka.
“Simba inaundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu na wachache wanaodaiwa kuwa ni watoto ambao wamekosa uzoefu, wasitafute sababu, wameweza kushinda, kutoka sare na timu hiyo na kufungwa wakiwa na timu hiyo, huko kote wasiseme watoto, wakikaribia na
Yanga wanadai kuwa ni watoto, hiyo si kutafuta sababu?” alisema Niyonzima.
Wachezaji wa Simba ambao wana uzoefu ni Juma
Kaseja, Abel Dhaira, Nassoro “Chollo” Masoud, Mussa Mude, Mrisho Ngassa,
Amri Kiemba, Felix Sunzu, Mwinyi Kazimoto, Haruna Chanongo na Shomari
Kapombe.
Kwa mujibu wa Niyonzima, Yanga ina wachezaji wengi
ambao umri wao hautofautiani na wanaodaiwa kuwa ni yosso wa Simba
watakaocheza nao Jumamosi jijini Dar es Salaam.
“Tuna kina Frank Domayo, David Luhende, Simon Msuva na wengine wengi, mbona sisi hatusemi ni watoto, waache kutafuta sababu,” alisema na kuwasisitiza mashabiki kuja uwanjani wakiwa wamejiamini na kuwashangilia kwa nguvu wawape raha na mvua ya mabao.
Haruna alisema wamejiandaa kupambana haswa kuibuka na ushindi na si lazima wapate mabao matano ila wanayataka. “Ushindi ni lazima, iwe mabao matano, zaidi ya matano, pungufu ya hayo, sisi kwetu ni muhimu kuwapa raha mashabiki na wala si vinginevyo."
Alifafanua kuwa wao hawadharau kikosi cha Simba na wanakichukulia kuwa ndicho sahihi; "Hao wachezaji wamewaondoa wao katika kikosi kwa maana hiyo wamekiamini kikosi chao, wasubiri matokeo yake kujua mwelekeo wao, sisi tupo tayari kwa mapambano."
Alisema kuwa hakutakuwa na maana ya Yanga kuwa
bingwa halafu wanafungwa na Simba katika mchezo ambao wanaamini kombe
litakuwa uwanjani tayari kwa makabidhiano.
“Tuna kikosi kizuri, nawaomba wachezaji wenzangu wasibweteke na ubingwa tulionao, kuifunga Simba ni kitu muhimu sana kuliko kitu chochote, mashabiki na wanachama wanataka kuona sisi tunawapa raha, hakuna mchezo siku hiyo,” alisema.
Licha ya maneno hayo ya Haruna, Mwanaspoti linajua jopo la
usajili la Simba linafanya nae mazungumzo ya mara kwa mara kumshawishi
asaini Simba kwavile mkataba wake na Yanga umemalizika na hajasaini mpya
ingawa kamati ya usajili ya Yanga imesisitiza tayari amesaini mkataba
wa miaka miwili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope alisema jana Jumatatu kuwa hawajafanya mazungumzo na Niyonzima.
"Nikiwa kama Mwenyekiti wa Usajili, nasema sijafanya mazungumzo na Haruna wala sijawahi hata kupeana naye salamu tu."
No comments:
Post a Comment