CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Kilosa
kimeendeleza ubabe wa ushindi kwenye chaguzi ndogo baada ya juzi
kunyakua viti vyote vya kitongoji na kijiji katika Kata ya Ruaha.
Uchaguzi huo ulifanyika kujaza nafasi hizo kutokana na waliokuwa wakizishikilia kufariki dunia na wengine kujuzulu.
Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, Rashid Kalembela, nafasi ya
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kifinga ilichukuliwa na Kilango Mshana
aliyepata kura 451 na kumbwaga Castory Manga wa CCM aliyepata kuwa 248.
Katika Kitongoji cha Ruaha ‘B’, George Banda wa CHADEMA aliibuka
mshindi kwa kura 428 dhidi ya Abdalah Kimbaa wa CCM aliyepata kura 155.
Akizungumzia ushindi huo, meneja kampeni wa wagombea wa CHADEMA,
Mathew Likwina, alisema matokeo hayo yalilazimishwa kusomwa saa 12 jioni
na umati wa watu baada ya kucheleweshwa makusudi.
Alisema mpango walionao sasa ni kuwaalika kwa gharama zao viongozi wa
chama taifa kuja kushuhudia wanavyosimikwa na kutoa nasaha juu ya mfumo
bora wenye tija katika kuongoza wananchi.
No comments:
Post a Comment