KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, walimu wapya wa shule za
sekondari wilayani Magu, mkoani Mwanza, juzi walilazimika kulala nje ya
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Magu, wakishinikiza
kulipwa mishahara yao.
Walimu hao wapatao 100 kutoka shule mbalimbali wilayani hapa,
walifikia uamuzi huo baada ya kutolipwa mishahara yao na haki zao
nyingine stahiki tangu Machi mwaka huu, walipoajiriwa na serikali.
Wakizungumza nje ya ofisi hiyo, walimu hao
walieleza kuchukizwa na kitendo cha serikali kutowalipa mishahara kwa
muda wote huo.
Walisema kuwa kati ya walimu wapya 154, ni walimu zaidi ya 50 pekee
ndio wameingizwa kwenye mpango wa kulipwa mishahara, huku wengine wakiwa
hawajui hatima yao.
Walifafanua kuwa ofisi ya mkurugenzi imekuwa ikikataa kuzungumza nao
na wakati mwingine inawaamuru waende kuomba fedha za kujikimu kwa wakuu
wao wa shule, jambo ambalo wakuu hao wanakataa.
“Licha ya kwamba mkurugenzi jana hatukumkuta na kupewa vitisho hivyo,
tulilazimika kuweka kambi na kulala hapa. Na leo hatutaondoka hapa mpaka
kieleweke,” alisema Deusdedith Millanzi kwa niaba ya wenzake.
Walimu hao waliongeza kuwa kutokana na kukosa mishahara yao tangu
waajiriwe Machi mosi mwaka huu, kwa sababu majina yao hayajaingizwa
kwenye utaratibu wa malipo, wataendelea kuweka kambi na kulala nje ya
ofisi hizo.
Walisema kuwa wamejionea mkanganyiko dhidi ya majina yao, ambapo
baadhi ya majina yaliyopo Ofisi ya Utumishi Wilaya ya Magu yanaonesha
hayamo kwenye mpango wa kulipwa.
Lakini kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya majina hayo yanaonesha yamo
katika mpango huo wa kupata mshahara kama watumishi wengine wa serikali.
“Tumechoka kuzunguka. Hivi tumeletwa Magu kuja kuteseka? Na kwa mtindo
huu wanatuweka kwenye mazingira magumu sana walimu wengi. Tutaishije
hawatulipi?” alihoji mwalimu mwingine ambaye alikataa kutajwa jina lake.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Magu (CWT), Boniphace
Maghembe, aliiambia Tanzania Daima kuwa madai ya walimu hao yapo sahihi
na kuitaka serikali iwalipe mishahara na stahiki zao si vinginevyo.
Akizungumzia malalamiko hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo
ya Magu, Bonaventra Kiswaga, alikiri walimu hao kulala nje ya ofisi ya
mkurugenzi wakishinikiza kulipwa mishahara yao.
Kiswaga alisema kulingana na unyeti wa madai ya walimu hao, ofisi ya
mkurugenzi na Utumishi ya wilaya hiyo zinayafanyia kazi malalamiko ya
walimu hao, hivyo kuwataka wavute subira wakati ufumbuzi wa tatizo hilo
ukitafutwa.
No comments:
Post a Comment