MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amewasilisha
ombi katika Mahakama ya Rufaa nchini, akiomba itengue uamuzi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wa kumfutia mashitaka matatu ya
ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Dk. Feleshi aliwasilisha ombi hilo juzi kwa njia ya maandishi, ambapo
katika maombi yake anaiomba mahakama hiyo iitishe mwenendo wa shauri
lililotolewa uamuzi huo na Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrence Kaduri Mei 8,
mwaka huu na kuupitia upya na ifute uamuzi huo kwa kuwa una makosa
kisheria.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Dk. Feleshi anadai Mahakama Kuu
haikuombwa kumfutia mashitaka Lwakatare kama Jaji Kaduri alivyotoa
uamuzi huo, bali aliiomba mahakama iitishe majalada ya kesi ya msingi
iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na 20 mwaka huu.
“Kwa kuwa Ofisi ya DPP ipo kwa ajili ya kusimamia utawala wa sheria,
haijaridhishwa na uamuzi wa Mahakama Kuu uliomfutia mashitaka matatu
Lwakatare, hivyo tunaiomba mahakama hii iitishe mwenendo wa kesi
ulioamuliwa, kwani tunaamini kisheria jaji alikosea kutoa uamuzi ule,
kwani Lwakatare hakuwa ameomba afutiwe mashitaka yanayomkabili,” alidai
Dk. Feleshi.
Hata hivyo hadi jana mchana uongozi wa Mahakama ya Rufaa ulikuwa bado haujapanga majaji wa kusikiliza ombi hilo.
Chanzo cha habari na Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment