SERIKALI hutoa ruzuku ya sh bilioni 36.7 kila mwaka kwa hospitali 97 za mashirika ya dini nchini.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alitoa kauli
hiyo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Muleba
Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), aliyetaka kujua ni kwanini serikali
isitumie hospitali za misheni kwa kuzipa ruzuku ya dawa na mishahara ya
watumishi, ili ziweze kutoa huduma bora na kwa gharama nafuu kwa
wananchi.
Aidha, mbunge huyo aliihoji serikali kama iko tayari kupandisha hadhi
zahanati ya Bumbile, ili iweze kuhudumia visiwa vya Bumbile, Kalebe na
Makibwa vilivyo mbali na hospitali za misheni za Ndolage, Rwantege na
Kagondo.
Akijibu swali hilo, Dk. Rashidi alisema ruzuku hiyo ni mbali na ile
iliyotolewa na halmashauri za mashirika ya dini kutoka katika mfuko wa
maendeleo na mishahara ya watumishi walioshikizwa katika hospitali hizo.
Sambamba na hilo, alisema serikali inaendelea kuboresha mazingira
yatakayoziwezesha hospitali hizo ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi
kwa gharama nafuu.
“Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inasimamia ubora na viwango katika
kutekeleza hili. Wizara imeweka vigezo vya utoaji huduma kwa kila
ngazi,” alisema Dk. Rashidi.
No comments:
Post a Comment