WANANCHI wilayani Bunda mkoani Mara wamelalamikia kitendo cha
Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (Bunda-DDH) kukosa barafu kwenye
chumba cha kuhifadhia maiti.
Walisema hali hiyo imekuwa ikiwalazimu watu wanaofiwa ndugu zao
kupeleka maiti katika hospitali za nje ya wilaya hiyo, zikiwemo
Hospitali ya Rufaa Bugando, Shirati, Tarime na Hospitali ya Mkoa wa
Mara iliyoko mjini Musoma.
Wakizungumza kwa nyakati na mwandishi wetu maeneo tofauti jana,
wananchi hao walisema hiyo ni kero kubwa na wamekuwa wakiingia gharama
kubwa.
Walisema chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Bunda-DDH
kwa kipindi kirefu hakina ubora kutokana na kutokuwa na jokofu la
kufanya maiti zisiharibike.
“Hii hospitali imeshapoteza umaarufu wake iliyokuwa nao wakati
inaanzishwa, chumba cha kuhifadhia maiti hakina ubora kabisa... hakuna
friji, tunaangaika kutunza miili ya marehemu, sasa tunaipeleka nje ya
wilaya kwa gharama kubwa,” alisema mwananchi mmoja wa mjini Bunda.
Aidha, walisema sio vema hospitali teule kukosa huduma hiyo na kwamba
pia kituo cha afya Manyamanyama, ambacho sasa kimepandishwa hadhi na
kuwa Hospitali ya Wilaya ya Bunda, pia hakina huduma hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Bunda-DDH, Dk. Karekamo, alisema tatizo hilo ni la muda
mrefu na kwamba linashughulikiwa.
No comments:
Post a Comment