Mkurugenzi
Mkuu wa Helvetic Solar Contractors Eng. Patrick Ngowi akiwa na mwenyeji
wake Mkurugenzi Mkuu wa ITV na Radio One Bi. Joyce Mhavile, alipofika katika
ofisi hizo kwa ajili ya mazungumzo na kuhojiwa katika kipindi
cha Business Edition, kitakachorushwa Ijumaa hii saa 2 na dakika 15
usiku, Capital TV. (Picha na habari na Amani Nkurlu.)
Dar es Salaam. 21 Mei, 2013 Mkurugenzi Mkuu wa
Helvetic Solar Contractors Eng. Patrick Ngowi ameendelea kutoa rai kwa
vijana nchini Tanzania kuwa na moyo na bidii ili kuweza kutimiza ndoto
zao za maendeleo na kujikwamua kiuchumi.Eng. Ngowi ambaye pia ni mshindi wa ‘Forbes 2013: 30 under 30: Africa’s Best Young Entrepreneurs’ alisema maneno hayo mapema leo katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa ITV na Radio One Bi. Joyce Mhavile alipofika kufanya ziara na mahojiano maalum katika kituo hicho.
“Vijana wa kitanzania wanafursa nyingi sana katika nchi yetu, imefika wakati sasa vijana wajitambue kwamba wanaweza kutimiza ndoto zao kadiri bidii zao zitakavyowatuma. Kwa mfano, mi nilianza na mtaji wa shilingi milioni mbili, lakini hivi sasa nilipofikia biashara yangu imekua na nimeweza kufanya maajabu makubwa katika soko ukizungumzia swala ya nishati ya jua,” alisema Eng. Ngowi.
Aliongeza, “Kinachotakiwa ni kuwa mbunifu katika biashara unayofanya, kuwa na ujasiri pamoja na umakini wa kile unachokipenda na pale unapotaka kufika. Yote yanawezekana na kijana yeyote anaweza fanikiwa.”
Pamoja na hayo Eng. Ngowi aliwapongeza sana IPP media kwa mafanikio yao waliyopata katika kipindi chote tangu kianzishwe, ikiwemo tuzo ya ‘Number 1 Super Brand’ katika Afrika Mashariki hivi karibuni.
Aidha,Mkurugenzi Mkuu wa ITV na Radio One Bi. Joyce Mhavile alimpongeza kwa mafanikio yake na kumshukuru sana Eng. Ngowi kwa ugeni wake.
Kampuni ya Helvetic Solar Contractors ambayo Eng. Ngowi ni muasisi wake, mwaka jana iliweza kushinda nafasi ya kwanza katika mashindano ya ‘100 Top Mid-Sized Company in Tanzania.’ Mwezi Machi mwaka huu Eng. Ngowi aliweza kuorodheshwa katika kundi la wajasiriamali bora 30 vijana barani Afrika wenye umri chini ya miaka 30 ijulikanayo kama ‘Forbes 30 under 30: Africa’s Best Young Entrepreneurs’.
No comments:
Post a Comment