HATIMAYE Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa kampuni ya Clouds
Media Group ya jijini Dar es Salaam, Ruge Mutahaba, amefungua kesi ya
madai dhidi ya mwanamuziki nguli, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, ambayo
inataanza kusikilizwa Mei 27 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.
Kupitia kwa wakili wake, Ruge amefungua madai dhidi ya Jay Dee kupitia
jalada namba 29/2013 chini ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Athuman
Nyamlani, ambaye pia ni Makamu wa Rais Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).
Hata hivyo, wakili wa Ruge ambaye alikuwa mahakamani hapo hakuwa
tayari kudokeza madai ya msingi ya mashtaka yaliyofunguliwa ingawa pande
hizo mbili zimekuwa kwenye malumbano ya maneno ambapo msanii huyo
alidai Clouds Media Group imekuwa hairushi matangazo ya bendi yake.
“Tumefungua kesi ya madai, zaidi mumtafute Jay Dee mwenyewe au Ruge
ndiyo wenye kuongelea; mimi siwezi kuongea chochote hadi
nitakaporuhusiwa na mteja wangu,” alisema wakili huyo ambaye hata jina
lake alikataa kuweka hadharani.
Awali mwandishi wa habari hizi aliweza kuwasiliana na Gadna G Habash
ambaye ni Meneja na Mume wa Mwanamuziki Lady Jay Dee, aliyekiri kupokea
taarifa ya kuitwa mahakamani kwa Jay Dee, ingawa hajui kwa ajili ya
nini.
“Ni kweli walifika watu na barua ambayo ni ya wito kwa Jay Dee ili
afike mahakama ya Kinondoni, Jumatatu (jana); hata hivyo hawakumkuta,
lakini wito huo amefikishiwa mlengwa,” alisema Gadna.
Gadna alisema hajajua Lady Jay Dee anaitiwa nini na amemwelezea na
amesema atatekeleza wito huo. Hata hivyo, wakati tunakwenda mitamboni,
kulikuwa na habari kuwa Gadna na Jaydee walifika mahakamni majira ya saa
sita mchana.
No comments:
Post a Comment