RAIA wa Kenya, Eric Njoroge Waisaka, amefariki dunia katika
mazingira ya kutatanisha kwenye Hoteli ya Sleep Inn iliyopo mtaa wa
Mahiwa na Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Tayari ndugu wa marehemu wameshawasili jijini Dar es Salaam, kwanza
kwa ajili ya kujua sababu za kifo na kushughulikia taratibu za kuuchukua
mwili huo huku viongozi wa hoteli wakitupiana mpira kuzungumzia tukio
la kifo chake.
Habari ambazo chanzo hiki kilizipata, zilisema kuwa raia huyo wa Kenya
aliingia hotelini hapo Jumamosi iliyopita na siku iliyofuata alikutwa
amekufa akiwa kwenye choo cha chumba alichofikia katika hoteli hiyo.
Meneja wa hoteli hiyo aliyejulikana kwa jina moja la Zarina,
alipopigiwa simu juu ya tukio hilo alisema hayupo katika nafasi nzuri ya
kuzungumzia kwa kuwa yupo msibani jijini Tanga.
“Mimi siku ya tukio nilikuwa nyumbani hivyo nimeambiwa kama wewe na
kwa sasa nipo msibani, Tanga tafadhali wasiliana na ofisini watakuwa na
jambo la kukueleza,” alisema Zarina.
Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Muslim Meghy, alipopigiwa simu alisema
suala hilo hawezi kulizungumzia kwa kuwa halijawa na uzito wa
kuzungumziwa katika nafasi yake.
Alimweleza mwandishi wa habari hizi awasiliane na meneja na
alipoambiwa kuhusu majibu ya meneja wake, mkurugenzi huyo aliomba
apigiwe simu siku iliyofuata, lakini hakuweza kupokea simu yake kila
alipopigiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema taarifa za awali zinaonesha mtu huyo
alizidiwa na shinikizo la damu.
Mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kisha kurejeshwa kwao Kenya kwa mazishi.

No comments:
Post a Comment