JESHI la Polisi Mkoa wa Kinondoni linamshikilia Conrad Leo kwa
tuhuma za kumpiga risasi na kumuua Ayoub Mlay (38), wakati wakiwa katika
klabu ya Ambrosia iliyoko Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wameliambia Tanzania Daima Jumapili
kuwa mtuhumiwa huyo alishawahi kupokonywa silaha yake kabla ya
kurudishiwa katika mazingira ya kutatanisha siku za hivi karibuni.
Inadaiwa kuwa sababu za awali zilizosababisha mtuhumiwa huyo
kupokonywa silaha hiyo na Jeshi la Polisi ni pamoja na matumizi mabaya
ikiwamo kuwatishia watu kila wakati wanapotofautiana kwa kauli.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo akisema kuwa mtuhumiwa akiwa katika klabu ya
Ambrosia jijini Dar es Salaam, alimfyatulia Mlay risasi katika eneo la
kifua, baada ya kutokea mabishano kati yao na kusababisha kifo chake.
Alisema taarifa juu ya mtuhumiwa huyo kuwahi kupokonywa silaha yake na
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni na baadaye kurejeshewa katika
mazingira ya kutatanisha hana uhakika nazo na aliahidi kufuatilia.
“Kwa sasa mtuhumiwa anashikiliwa katika kituo cha Polisi Kawe na
tutachunguza hilo la kunyang’anywa bastola na kama lipo tutaangalia
sababu za msingi za kurudishiwa silaha hiyo katika mazingira
yanayoelezwa kuwa ya kutatanisha,” alisema Kenyela.
No comments:
Post a Comment