WATUHUMIWA wanne wa tukio la mlipuko wa bomu katika Kanisa
Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti la jijini
Arusha kutoka Nchi za Falme za Kiarabu (UAE) na nchi ya Saudi Arabia
hatimaye wameachiwa huru baada ya timu ya uchunguzi kujiridhisha
kutokuhusika kwao na tukio hilo.
Raia hao wa kigeni waliokuwa wakihojiwa kwa wiki moja sasa mara baada
ya kutokea kwa tukio hilo ni pamoja na Abdul Aziz Mubarak (30) ambaye ni
mfanyakazi wa mamlaka ya mapato, Fouad Saleem Ahmed Al Hareez al Mahdi
(29) mfanyakazi wa kikosi cha zimamoto na Saeed Abdulla Saad (28) ambaye
ni askari polisi kitengo cha usalama barabarani wote ni kutoka Nchi ya
Falme za Kiarabu (UAE).
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoa Arusha Liberatus Sabas mtuhumiwa
mwingine ni Al-Mahri Saeed Mohseen (29) ambaye ni raia wa Saudi Arabia.
Raia hao wanne wote kwa pamoja waliachiwa huru baada ya timu ya
uchunguzi inayojumuisha jeshi la polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), taasisi ya kigeni ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na
Interpol kubaini ya kwamba raia hao wa kigeni hawakuhusika na tukio hilo
la kigaidi.
“Uchunguzi wa kina uliofanywa na timu ya upelelezi ukihusisha polisi
na taasisi za upelelezi FBI pamoja na Interpol kuhusiana na tukio hilo
la mlipuko wa bomu kanisani umebaini kuwa raia hao wanne wa kigeni
hawahusiki katika shambulio hilo,” alisema kamanda Sabas.
Waliokufa katika tukio hilo la kigaidi lililotikisa jiji la Arusha ni
Regina Loning’o Kurasei (50) mkazi wa Olasiti, Patricia Joachim (9)
Mkazi wa Majengo aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu shule msingi
Elerai na James Gabriel (16) mkazi wa Olasiti aliyekuwa mwanafunzi wa
kidato cha tatu katika shule ya sekondari Arusha Day.
Aidha alisema jalada la tukio hilo lilipofikishwa kwa mwanasheria mkuu
wa serikali kanda ya Arusha divisheni ya mashtaka alielekeza kuwa
watuhumiwa wakabidhiwe ofisi ya idara ya uhamiaji mkoa wa Arusha ili
kuona kama kuna taratibu zozote za kiuhamiaji zilikiukwa na wageni hao
walipoingia nchini ili hatua stahiki zichukuliwe.
Alisema ofisi hiyo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mashtaka
dhidi ya mtuhumiwa wa kwanza Victor Ambrose Kalisti (20) ambaye
alifikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi jana kwa tuhuma za mauaji na
kujaribu kuua ambapo kamanda Sabas alieleza kuwa uchunguzi dhidi ya
watuhumiwa waliobakia bado unaendelea na timu ya upelelezi imeongozeka
kwa wataalamu kutoka Kenya na Uganda nao wameingia nchini.
Watuhumiwa waliobaki ni pamoja na Yusuph Lomayani (18), George
Bathlomeo Silayo (23), Mohamed Suleiman Saad (38) mkazi wa Ilala Dar es
Salaam, Jassin Mbarak (29) pamoja na wengine ambao hakuwataja katika
taarifa yake ya jana.
Kamanda alieleza ya kwamba majeruhi wa mlipuko huo wa bomu uliotokea
katika kanisa hilo Jumapili iliyopita na kuna watu watatu na kujeruhi
wengine wamebaki majeruhi 31 ambao kati yao 19 wanatibiwa katika
Hospitali ya Mount Meru ya jijini hapa wengine wanne hospitali ya st.
Elizabeth wengine wanane wako hospitali ya taifa Muhimbili jijini Dar es
Salaam na hali yao inaendelea kuimarika.
Hata hivyo timu ya upelelezi inaendelea kufuatilia taarifa ya
watuhumiwa wanaohusishwa na tukio hilo ili mkondo wa sheria uchukuliwe
na amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za siri haswa ikizingatiwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Saidi Mwema, ameshatangaza donge
nono la sh 50 milioni.
No comments:
Post a Comment