WALEMAVU wasiosikia wamelalamikia kutopata haki ya habari katika
vituo vya televisheni kutokana na kukosekana kwa wataalamu wa lugha za
alama.
Walemavu hao walitoa kilio hicho jijini Dar es Salaam jana wakati
Klabu ya Waandishi Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) walipotembelea
makundi ya maalumu yale ya walemavu na watoto waishio katika mazingira
maalumu katika kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Walisema vitu ambavyo vinatokea huko wao hawajui kutokana na
kutokuwapo na wataalamu wa lugha ya alama ambao ndio wangekuwa
kuwafikishia taarifa kwa njia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Shule ya Viziwi
Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Kuwahudumia Viziwi Tanzania na Kaimu
Mkurugenzi wa Shule ya Msingi Buguruni-Viziwi- Yassini Mawe, alisema
suala la habari linaonekana halipewi kipaumbele kwa kundi hilo.
Alisema kuwa wamepata elimu ya kutosha katika uchaguzi wa Kenya kwa
kuwa kulikuwapo na wataalamu wa lugha ya alama kwenye vituo vya
televisheni.
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Dar es Salaam
(DCPC), Benjamin Masese, alisema maadhimisho hayo yawe chachu kwa jamii
katika kutoa habari zao, ili ziweze kufikika katika mamlaka husika.
Wakati huohuo, Kambi ya Wazee ya Nunge, Kigamboni ilikataa msaada
pamoja na kuzungumza na waandishi wa habari kwa madai kuwa viongozi wa
klabu ya waandishi hawakutoa taarifa ya ujio wao, hivi kulazimika
kupeleka msaada huo kwa watoto waishio katika mazingira magumu katika
kituo cha Songambele Pamoja.
Wakati huohuo, waandishi wa habari nchini, wamesema uhuru wa vyombo
vya habari nchini hauwezi kupatikana bila kuwepo utaratibu maalumu
unaowafanya waweze kunufaika na taaluma yao.
Mwandishi wa Redio Uhuru, Cosmas Hinju, alisema waandishi wa habari
wamekuwa kama ‘punda’ kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa wakati
muafaka, hali inayowafanya kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo
rushwa.
Mhariri wa mtandao wa habari mpya.com, Odoyo Jackson, alisema uhuru wa
vyombo vya habari nchini uko mashakani kwa kuwa baadhi ya wanahabari
wameingia kwenye vikundi vya siasa.
Mwandishi wa gazeti la Mtanzania, Arodia Peter, alisema anaiona siku
hiyo kama kiza kinene kwa kuwa waandishi wa habari hawana uhakika na
maisha yao, kwani kuna makundi ya watu wameziweka roho za wanahabari
rehani.
No comments:
Post a Comment