MTANDAO wa watetezi wa haki za binadamu nchini wameelekeza 
tuhuma kwa serikali katika masuala mbalimbali yahusuyo utendaji huku 
wakiilaumu kuwa imeshindwa kuongoza vema.
Badala yake wamesema serikali imeanza kutishia wanaharakati na 
waandishi wa habari na hali hiyo imesababisha wananchi kuanza 
kujichukulia sheria mikononi.
Katika tamko lao la kufunga mafunzo yao yaliyofanyika jijini Dar es 
Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, watetezi hao walisema  kushamiri kwa
 vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi, kuteka, kutesa, kung’oa 
meno, na macho, kukata vidole na hata kuwarushia mabomu waamini wakiwa 
katika maeneo ya maombi, ni ishara ya serikali iliyoshindwa kutimiza 
majukumu yake.
Badala yake imewekeza katika matumizi ya nguvu kuwakandamiza watetezi 
wa haki za binadamu kwa namna mbalimbali, ikiwemo kuwafungulia kesi huku
 watetezi wakishutumiwa kuwa ni wapinzani kwa sababu kazi zao zimekuwa 
zikilinganishwa na kazi za vyama vya upinzani na za kiuchochezi.
  Watetezi hao wameiasa serikali ielewe kuwa watetezi ni kiungo muhimu 
katika kuibua na kufichua maovu ili kujenga utawala unaoheshimu haki za 
binadamu.
Aidha, katika tamko hilo waliongeza kuwa  wanahabari wanakabiliwa na 
changamoto nyingi za kiusalama huku  wamiliki wa vyombo hivyo wakiwa 
hawana mikakati mizuri ya usalama wa waandishi wao.
“Pia malipo finyu kwa wanahabari ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa 
kuharibiwa kwa habari za kweli kwa sababu baadhi yao hawapati malipo ya 
uhakika wala mikataba,” lilisema tamko hilo.
Wanaharakati hao pia wameliasa Jeshi la Polisi liwe makini kuepuka 
matumizi ya silaha za moto na nguvu za ziada ambazo zimekuwa 
zikisababisha vifo na ulemavu wa kudumu.
  “Katika purukashani nyingi za kisiasa jeshi hilo limeshindwa kabisa 
kuonyesha kwamba linafanya kazi ya kuutumia umma wa Watanzania wote na 
badala yake limekuwa likichukua mwelekeo wa kuwatumikia wanasiasa au 
chama fulani,” ilisema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment