KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha
Kilimanjaro Premium Lager, imewazadia sh milioni 25 mabingwa wa Ligi Kuu
Tanzania Bara, Yanga, kwa kutwaa taji hilo.
Mbali na zawadi hiyo ya TBL, Yanga ilijihakikishia kitita cha sh
milioni 70 kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi hiyo, kampuni ya simu za
mikononi ya Vodacom, kwa kuibuka mabingwa.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Meneja wa bia ya
Kilimanjaro, George Kavishe, alisema kwamba zawadi hiyo ni sehemu ya
ahadi ya udhamini wao kwa timu itakayoshinda au kushika nafasi za juu.
“Kama wadhamini wa klabu kongwe za Yanga na Simba, tuliahidi kutoa sh
milioni 25 kwa timu itakayotwaa ubingwa wa Ligi Kuu na sh milioni 15 kwa
timu itakayoshika nafasi ya pili, hivyo kutokana na Yanga kutwaa
ubingwa ndio tunaikabidhi fedha hizi,” alisema.
Kavishe aliongeza kuwa zawadi hiyo ni sehemu ya sh bilioni 1.5 za
udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga na imetolewa kwa lengo
la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa kushinda zaidi na kusaidia katika
maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
“Na tulifanya hivi makusudi ili kuleta ushindani kwa timu hizi za
Simba na Yanga, ili ziweze kufanya vema kwenye ligi hiyo ambayo imekuwa
na ushindani mkubwa.
Yanga imekuwa ikicheza mpira mzuri kipindi chote cha msimu wa Ligi Kuu na hivyo kuibuka washindi.
Napenda kuwapongeza wachezaji, kocha na uongozi mzima wa Yanga kwa
matokeo mazuri ya kushinda Ligi Kuu kwa mara ya 24 sasa,” alisema
Kavishe.
Akipokea hundi hiyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, mbali
ya kushukuru,
alisema timu yao ni nzuri na yenye nguvu kutokana na
uongozi imara, pamoja na udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager.
“Mafanikio yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio pia ya bia ya
Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla, ambayo imekuwa ikitusaidia sana.
Bia hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuipa timu msukumo uliopelekea
mafanikio haya,” alisema.
Kwa ubingwa huo, Yanga itaiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa
Afrika mwakani, pamoja na michuano ya Kombe la Kagame, ambalo ni
mabingwa watetezi.
No comments:
Post a Comment