UBORA wa klabu kongwe za Simba na Yanga, umeifanya timu ya
Sofapaka kutoka Kenya kuleta kikosi chake chote ili kukabiliana nazo
katika michezo ya kirafiki itakayopigwa hapa nchini.
Sofapaka kutoka Kenya.
Sofapaka inatarajiwa kutua nchini Juni 10 kwa ziara ya kimichezo,
ikiwa na lengo la kuzipima klabu hizo kongwe zitakazokuwa katika
maandalizi ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe
la Kagame, itakayoanza kutimua vumbi Juni 18 hadi Julai 2, huko Sudan
Kusini.
Akizungumza kwa simu kutoka Kenya, Meneja wa Sofapaka, Ngalambe
Roberto, alisema kwamba hawana budi kuleta kikosi kamili ili kushinda
michezo yake.
“Sisi tumejiandaa vizuri, tunazifahamu na kusoma kwenye mitandao
kuhusu timu hizi, hivyo tutakuja na majeshi yote ili tushinde mechi zote
mbili,” alisema Ngalambe.
Alisema Tanzania kuna timu nyingi nzuri zenye ushindani, lakini kwa
Simba na Yanga ni zaidi, hasa kutokana na upinzani mkubwa uliopo kwa
timu hizo mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Smartsports, iliyoandaa
ziara hiyo, George Wakuganda, alisema Sofapaka itacheza mechi yake ya
kwanza Juni 12 dhidi ya Simba, kabla ya Juni 13 kukwaana na Yanga. Mechi
zote zitapigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment