BENKI ya Exim imeibuka mshindi wa jumla kwa taasisi za fedha
kwenye Tuzo za Mazingira zilizoandaliwa na Manispaa ya Ilala kwa mwaka
2013.
Tuzo hizo zinalenga kutambua michango ya taasisi mbalimbali nchini
katika utunzaji wa mazingira, ambapo sherehe za utoaji wa tuzo hizo
zilifanyika kwenye viwanja vya Mbagala Zakhem, wilayani Temeke.
Utolewaji wa tuzo hizo ulifanyika wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Mazingira iliyobeba kaulimbinu ya ‘Fikiri, Kula, Tunza’.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said
Meck Sadiki, aliitahadharisha jamii kutunza mazingira wanayoishi ili
kuwa na miradi endelevu.
Kwa mujibu wa Sadick, Dar es Salaam inakabiliwa na changamoto
mbalimbali katika masuala ya utunzaji wa mazingira, ukiwamo usimamizi
hafifu wa sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira.
“Hatuna budi kutii sheria hizi bila shuruti na tukifanya hivyo Dar es
Salaam yetu itakuwa sehemu nzuri na salama ya kuishi,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim, Anthony Grant, mara baada
ya kupokea tuzo hiyo alibainisha mikakati na jitihada za benki yake
kuunga mkono kampeni mbalimbali za utunzaji wa mazingira nchini.
“Benki ya Exim itaendelea kuunga mkono jitihada za mapinduzi ya uchumi
wa kijani. Tunahitaji kuiacha sayari hii ikiwa na mazingira
endelevu kwa vizazi vijavyo.
“Mabadiliko makubwa yanatakiwa kufanyika haraka kama tunahitaji kupiga
hatua kweli. Lazima matendo yetu na maamuzi ya kimazingira tunayofanya
yalete mabadiliko ya kijamii na kiuchumi katika maisha ya kila mmoja
wetu,” aliongeza Grant.
No comments:
Post a Comment