WANAFUNZI wa kidato cha tano na sita wa Sekondari ya kutwa
Ileje wamelalamikia kitendo cha walimu wao kushindwa kuingia darasani.
Akizungumza na CHANZO CHA HABARI, mmoja wa wanafunzi hao ambaye hakutaka
kutajwa jina lake alisema kuwa walimu wamekuwa wavivu wa kuingia kwenye
vipindi, ambapo tangu Januari hadi sasa (Juni) mwalimu mmoja ameingia
darasani mara tatu.
Chanzo hicho kilisema kuwa walimu wa masomo ya kawaida hawafundishi
huku wakidai kuwapo kwa uhaba wa walimu wa sayansi ambapo imekuwa vigumu
kujifunza kulingana na hali halisi ya mazingira ya shule hiyo.Kwa
upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Gwakisa Mwakyeja, alikiri kuwapo kwa
tatizo la walimu shuleni hapo na kudai kuwa atafuatilia kwa kina
maendeleo ya shule hiyo.
Mwakyeja alisema kuwa tatizo lililopo katika shule hiyo ni kuwa na
walimu wachache, hivyo wanajitahidi kufanya kila mbinu kuhakikisha
wanafunzi hao wanapata vipindi kila siku.
“Tatizo la walimu kwa shule hii lipo pia kwa nchi nzima, hivyo ni
tatizo la kitaifa, hivyo nimeshukuru hata kupewa hawa walimu japo ni
wachache na nitazidi kukabiliana na changamoto hiyo kuhakikisha kuwa
tunawapatia elimu ya kutosha,” alisema Mwakyeja.
Hata hivyo Ofisa Elimu Sekondari, Jimmy Nkwamu, alisema itabidi kuwa
na upembuzi wa kindani ili kuweza kuwabaini walimu wanaotoroka darasani
huku wakichukua mshahara kila mwisho wa mwezi.
No comments:
Post a Comment