MSANII mahiri wa muziki wa asili nchini, Chigwele Che Mundugwao
(46), na wenzake watatu jana walifikishwa katika mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la
wizi wa pasipoti 26.
Che Mundugwao anashtakiwa na wenzake, Ofisa Manunuzi wa Idara ya
Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na
Uokoaji, Kenneth Pius (37), na mfanyabiashara, Ally Jabir (34).
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladislaus Komanya, mbele ya Hakimu
Mkazi Aloyce Katemana, alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la
kula njama kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 384 cha Sheria ya
Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.
Wakili Komanya alieleza kuwa kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu,
Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma, makao makuu ya Idara ya Uhamiaji,
aliiba paspoti 26 mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Komanya alidai kuwa washtakiwa Chigwele, Kenneth na Ally, Mei 30
mwaka huu huko Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam, walikamatwa
wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.
Kuhusu Che Mundugwao, wakili Komanya alidai kuwa mshtakiwa huyo
Aprili 22, mwaka huu, alikamatwa akimiliki paspoti 12 za watu wengine,
bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi.
Wakili huyo aliendelea kudai kuwa Mei, mwaka huu, Che Mundugwao, pia
alikamatwa na maofisa wa usalama akimiliki pasipoti nyingine mbili
zenye majina ya watu wengine bila ya sababu yoyote ya msingi.
Komanya aliendelea kudai kuwa Aprili 24, mwaka huu, mshtakiwa Ally
alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha kuwa ilikuwa ni halali
na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji, wakati akijua kuwa si kweli.
Wakili Komanya alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,
Shemweta alighushi nyaraka za serikali, ambazo ni muhuri akijaribu
kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na
Idara ya Uhamiaji, wakati si kweli.
Baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka hayo, walikana na upande wa jamhuri ukadai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Wakili Komanya alidai kuwa kutokana na asili ya makosa hayo,
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, aliwasilisha hati ya
kuzuia dhamana chini ya kifungu cha 148 (4) cha sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 na ataiondoa hati hiyo, pale atakapoona
ipo sababu ya kufanya hivyo, ila kwa sasa amefunga dhamana ya washtakiwa
hao.
Kiongozi wa jopo la mawakili wanaowatetea washtakiwa hao, Peter
Kibatala, aliiomba mahakama kuwapa dhamana kwa sababu mashtaka yao
yanadhaminika na kwamba hayapo katika vifungu ambavyo vinazuia dhamana.
Hata hivyo, Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 5,
mwaka huu, kwa ajili ya kutoa uamuzi juu ya hoja hizo zilizowasilishwa
mahakamani hapo na akaamuru washtakiwa wote wapelekwe mahabusu.
No comments:
Post a Comment