
Zaidi ya wasanii 100 wametajwa kuwania tunzo hizi, na wote wana imani
ya ushindi na watakuwa ukumbini leo pamoja na baadhi ya mashabiki wao,
kushuhudia matokeo ya kazi ngumu waliyoifanya katika msimu uliopita wa
muziki wa Tanzania.
Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro,
kilichodhamiria kupeleka muziki wa Tanzania katika kilele cha mafanikio,
leo ndiyo mwenyeji wa shughuli husika na wameahidi usiku wa kihistoria,
huku wakiadhimisha mwaka wa 13, wa tunzo hizi ambazo kila kukicha
zinazidi kujizolea umaarufu.
George Kavishe, ni Meneja wa bia ya Kilimanjaro na amefanya mahojiano
na gazeti hili kuhusiana na usiku wa leo na mambo muhimu makubwa matatu
yametajwa katika kuunogesha usiku mwingine wa tunzo, uliokuwa
ukisubiriwa kwa hamu.
Kwanza, usiku hautakuwa Dar es Salaam peke yake utakuwa katika mikoa
ya Mwanza, Kilimanjaro na Dar ambapo katika viwanja mbalimbali vya Taifa
Dar es Salaam, Mabatini Mwanza, na CCM Mkoa kwa Kilimanjaro kutakuwa na
TV kubwa zitakazokuwa zikionyesha moja kwa moja tukio la utoaji tunzo
litakalokuwa likiendelea katika Ukumbi wa Mlimani City usiku wa leo.
Watazamaji wa mikoani, watashuhudia tunzo hizo kwa kiingilio cha bia
moja tu milangoni, na wakiingia katika viwanja hivyo watakuta maandalizi
mazuri kutoka kampuni ya bia Tanzania, na watakuwa wakishuhudia onesho
lote, pamoja na burudani mbalimbali zitakazokuwa zinatolewa na
waandaaji.
Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam watakaopata bahati ya
kuhudhuria onesho hilo ambapo kiingilio kitakuwa Sh 75,000 kwa watu
maalumu na kawaida itakuwa Sh20,000.
“Sababu mbili za msingi za kuweka onesho hili uwanjani, kwanza, ni
kutokana ma mfumo wa digitali, ambapo Watanzania wengi wameshindwa
kukabiliana nao kutokana na hali ya kiuchumi, hivyo tumewapa fursa
nyingine ya kushuhudia tunzo, lakini pia tungependa mashabiki wakae
pamoja na kushuhudia tukio hili la kihistoria,” alisisitiza George
Kavishe.
Red Carpert
Hili ni zoezi litakalohusisha mastaa hasa upande wa
mitindo, ambapo picha zitakuwa zikichukuliwa, katika kuperuzi nani kaja
vipi na kavaa nini na alikuwa amesindikizwa na nani.
Hii itakuwa na mtangazaji wake na itakuwa ni kama sehemu ya kipindi
cha TV na kwa habari tulizonazo, ni kwamba mtangazaji wa Channel O na
mdau mkubwa wa burudani, Jokate Mwegelo ndiye atakuwa mwendeshaji.
Kwa mujibu wa waandaaji, zoezi litachukua kama saa limoja hivi, maana shughuli yenyewe itaanza saa mbili usiku.
Burudani
Itakuwa katika makundi manane, lakini si burudani ambayo
umewahi kuiona mahala popote pale, ni burudani itakayozingatia kauli
mbiu ya tunzo hizo kwa mwaka huu, kikwetukwetu.
Kwa mujibu wa Kavishe ni kwamba kamwe, hutaona mwanamuziki akiimba
wimbo wake uliouzoea, au unaouona akiuimba kila siku, pale atakuwa
katika mwonekano mwingine na ni burudani ambayo mwisho ni itakusisimua
uhisi kwamba umesogea hatua moja tangu uanze kuburudishwa na sanaa ya
muziki wa jukwaani.
Kavishe amethibitisha kwamba hakuna mwanamuziki wa nje aliyehusishwa
na burudani za muziki wa Kili mwaka huu, burudani nzima itakuwa
ikiendeshwa na wanamuziki wa nyumbani.
Wanaotajwatajwa...
Wanamuziki Ben Pol, Vanessa Mdee na Ommy Dimpoz wametajwa sana na mashabiki kwamba huenda ukawa ni mwaka wao kwa mujibu wa tunzo hizo na hii ikaja baada ya kuonekana kutajwa mara nyingi sana katika kuwania tunzo hizo.
Wanamuziki Ben Pol, Vanessa Mdee na Ommy Dimpoz wametajwa sana na mashabiki kwamba huenda ukawa ni mwaka wao kwa mujibu wa tunzo hizo na hii ikaja baada ya kuonekana kutajwa mara nyingi sana katika kuwania tunzo hizo.
Mmoja kati ya mashabiki wakubwa wa muziki na mdau, Poti Poti kutoka
maeneo ya Kawe, jijini Dar es Salaam ameliambia Mwananchi kwamba mwaka
huu wanamuziki hao huenda wakaigeuza kabisa historia ya muziki wa kizazi
kipya kutokana na kazi yao nzuri waliyoifanya mwaka jana.
Ben Pol, mpaka sasa anashikilia tunzo ya mwanamuziki bora wa R&B
ambapo Vanessa Mdee ni mwanamuziki mpya kabisa kwenye tasnia ya muziki
na ni mmoja kati ya wanamuziki wanaowania tunzo ya mwanamuziki
chipukizi.
No comments:
Post a Comment