MAZISHI ya msanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Albert
Mangwair, yaliyofanyika makaburi ya Kihonda-Kanisani, jana yaliutikisa
mji wa Morogoro mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Joel Bendera.
Shughuli hiyo ilitanguliwa na kuaga mwili na ilifanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri kutokana na wingi wa maelfu ya watu.
Hapa
jeneza la Ngwair linaingizwa karubini, ikiwa ni picha inayoonyesha kuwa
hatutaweza tena kukutana na msanii huyu hapa chini ya jua. R.I.P
Ngwair
Wingi wa watu ndio uliifanya Kamati ya Mazishi chini ya Adam Juma,
ihamishie hafla hiyo Uwanja wa Jamhuri badala ya nyumbani kwa usalama
zaidi.
Mji wa Morogoro ulianza kuzizima tangu asubuhi, baada ya kushuhudia vikundi vya
watu wengi vikielekea Jamhuri wakiwa kwa miguu, pikipiki, baiskeli na wengine kwenye magari vikienda na kurudi.
Wasanii na viongozi mbalimbali, akiwamo Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi ‘Sugu’, nao walikuwapo kwenye tukio la kuaga mwili wa Ngwair na
baadaye kwenye mazishi yake ambayo yalizua mkanyagano wa aina yake.
Idadi kubwa ya watu ilijitokeza katika shughuli ya kumuaga marehemu,
ambapo pia ilikimbilia makaburini kwa ajili ya kushuhudia mwili wake
ukiingia kaburini.
Awali, Mkuu wa Mkoa Morogoro, Joel Bendera, alifika nyumbani kwa mama
wa marehemu saa nne za asubuhi na kupata fursa ya kuwapa pole wafiwa.
Akizungumza na wanafamilia na baadaye Uwanja wa Jamhuri, Bendera
alisema Tanzania imepoteza msanii nyota na mwenye bahati ya kupendwa na
watu wengi.
“Hii ni hatari kubwa maana Ngwair ameonyesha ni kiasi gani alikuwa
nyota katika tasnia ya muziki wa Hip Hop kwa umahiri wake, sambamba na
kuishi na watu vizuri.
“Hii leo ni historia katika mkoa wa Morogoro, hususan kwa kushuhudia
watu wengi wakiwa na huzuni katika kumuaga msanii wao mpendwa kwa namna
moja au nyingine, hivyo serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto
zinazowakabili vijana hawa,” alisema Bendera.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, alisema wasanii wamechoka
kuishi kimaskini wakati watu wengi wanaheshimu kazi zao.
“Inaumiza kuona tunazikwa kwa mtindo huu wakati maisha yetu ni magumu
mno, hivyo hatuwezi kuona hali hii inaendelea kuota mizizi, hivyo
wasanii tuendelee kuwa makini katika hili.
“Matatizo yaliyompata Ngwair katika maisha yake ni sehemu ya
changamoto zilizopo katika tasnia hii ya muziki wa kizazi kipya, ingawa
tukifa mazishi yetu yanakuwa ya heshima mno,” alisema.
Pamoja na kukusanya watu wengi, watu wengi walionekana kwenda uwanjani
kuwaona wasanii wengine, hivyo kusababisha mkanyagano kila anapoingia
au kutoka msanii nyota.
Baadhi ya wasanii wenye majina makubwa walikuwa Wema Sepetu aliyelazimika kujificha kila wakati kutokana na mayowe ya watu.
Hata hivyo, matatizo yalianza kujitokeza wakati wa kuaga mwili
kutokana na askari kushindwa kukabiliana na wingi wa watu katika
kuwadhibiti.
Wakati wa shughuli ya kuaga, ghafla, rafiki wa Ngwair, aliyopata
matatizo naye Afrika Kusini, Mgaza Pembe, M 2 The P, aliletwa uwanjani
hapo kumuaga Ngwair.
Baada ya kuona muda unazidi kwenda na watu hawaishi, shughuli ya kuaga
ilikatishwa na kuanza msafara kuelekea makaburini, Kihonda Kanisani.
Barabara zilizopitiwa na msafara wa mwili wa Ngwair, zilikuwa zimejaa
watu wakiwa na nia ya kumungalia nyota wao akielekea nyumba yake ya
milele baada ya kufariki Afrika Kusini, Jumanne ya wiki iliyopita.
Kufika makaburini, umati mkubwa wa watu ulikuwapo, hivyo ndugu wa
marehemu kukosa muda wa kutia mchanga katika kaburi, hasa pale watu
waliposhindwa kusogea.
Kaka wa marehemu, Kenneth Mangwea, aliwashukuru Watanzania kwa moyo
wao wa upendo kiasi cha kushirikiana na wao kuhakikisha kuwa mwili wa
Ngwair unazikwa Tanzania.
“Nashukuru sana, natumia muda huu kuwatakia upendo zaidi na zaidi
Watanzania wenzetu, sambamba na kumtakia mapumziko mema huko mbinguni
Ngwair,” alisema Kenneth.
Hatari kubwa ilijitokeza makaburi ya Kihonda Kanisani, kutokana na barabara kufurika watu na hata eneo la makaburi.
Mwili wa Mangwair ulizikwa majira ya saa tisa za mchana, ikiwa ni siku
moja tangu aagwe kwenye Viwanja vya Leaders, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment