MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (CHADEMA), amesema marais
wanaoshindwa kutekeleza ahadi zao mpaka wanapomaliza vipindi vyao vya
uongozi washitakiwe.
Lyimo alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiuliza swali la nyongeza
ambapo alisema wabunge wengi hususan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wanalalamika kwa kutotekelezwa kwa ahadi za marais na kutaka wapelekwe
mahakamani walishindwa kufanya hivyo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi, alisema katika ahadi za rais hakuna mtu wa
kushitakiwa na kwamba ahadi zinazotolewa na hutekelezwa na serikali.
“Ahadi inayotolewa na rais utekelezaji ni jukumu la serikali na fedha
inatoka serikalini haitoki mfukoni mwa rais sasa hapa hakuna wa
kushitakiwa, kwani rais aliyepo madarakani akiondoka atakuja mwingine
ambaye ataendelea na utekelezaji wa ahadi zilizobakia,” alisema Lukuvi.
Alisema serikali kwa kadiri ya uwezo wake imejitahidi kutekeleza ahadi mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa juu serikalini.
Awali katika swali la msingi Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula (CCM)
alitaka kujua hatua zilizochukuliwa hadi sasa katika utekelezaji wa
ahadi ya rais ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Mkinga pia alitaka kujua
ni lini utekelezaji wa ahadi za rais utakamilika.
“Wakati wa ziara yake wilayani Mkinga, rais aliahidi kujengwa haraka
Hospitali ya Wilaya ya Mkinga kutokana na kukipandisha hadhi Kituo cha
Afya Maramba ili kitoe huduma za hospitali ikiwamo upasuaji, utekelezaji
wa ahadi hizo umefikia wapi?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Seif Rashid, alikiri
kwamba katika mwaka 2010 rais alipotembelea wakazi wa Mkinga aliahidi
kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Maramba ili kiweze kutoa huduma za
dharura lakini pia aliahidi kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya
Mkinga.
“Hata hivyo katika kutekeleza ahadi hizo serikali imetumia jumla ya sh
milioni 132.1 kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Maramba ili
kiweze kupandishwa hadhi na kutoa huduma bora zinazoendana na
hospitali,” alisisitiza naibu waziri huyo.
“Kazi zilizofanyika ni upanuzi wa eneo la kituo hicho kwa kuhamisha
makazi ya watu wanne na kuwalipa fidia, kufanya ukarabati wa chumba cha
upasuaji, kuweka upya mfumo wa umeme na maji taka, kununua kontena kwa
ajili ya kutengeneza chumba cha mapokezi na kununua mashine ya dawa ya
usingizi na mashine ya kufua nguo,” alisema Dk. Rashid.
Kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkinga, alisema imeshatoa sh milioni 221.4, ambapo sh milioni 21 zimetumika.
Aidha, alisema kwa sasa Kituo cha Afya cha Maramba kinatoa huduma zote
muhimu isipokuwa upasuaji kwa wajawazito na chumba cha upasuaji kipo
katika hatua ya mwisho ya ujenzi na kinatarajiwa kukamilika kabla ya
Julai mwaka huu.

No comments:
Post a Comment