MADAKTARI bingwa wa upasuaji wa tundu dogo kutoka Misri wametua
nchini kwa ajili ya kuwafanyia upasuaji wagonjwa walio kwenye Hospitali
ya Taifa Mumbili (MNH) na kuwapa uzoefu madaktari wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa kuwatambulisha
madaktari hao Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi,
alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwapa uzoefu madaktari wa hapa nchini
kwa kuwa huduma hiyo hapa bado haijaanza.
“Madaktari wa hapa nchini watanufaika kwa kupata mafunzo ya kitaalamu
ya upasuaji wa tundu dogo, yatakayotolewa na madaktari bingwa kutoka
nchini humo na baadhi ya wagonjwa waliochaguliwa kwa sababu maalumu za
kitabibu nao watanufaika,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema hiyo si mara ya kwanza kwa Tanzania na Misri kushirikiana
katika masuala ya afya, kwani madaktari wao wamekuwa wakitoa huduma
sehemu mbalimbali nchini, hasa katika utaalamu ambao madaktari wetu
hawana.
Alisema timu hiyo ya madaktari inajumuisha madaktari sita wa upasuaji
na wataalamu wawili huku akiishukuru nchi ya Misri kwa kuwa na moyo wa
kuwasaidia Watanzania hasa sekta ya afya.
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Donan Mmbando, alisema madaktari
hao watakuwa katika hospitali ya Muhimbili na wagonjwa watakaopata
bahati ya kuhudumiwa ni wale ambao walikwishaandaliwa kwa mujibu wa
taratibu za kidaktari.
Naye balozi wa Misri nchini, Hossam Omar, alisema amefurahi kuona
wanashirikiana na Watanzania na kwamba ushirikiano huo hautaishia hapo
huku akiahidi huduma nyingine zaidi hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment