Ni miaka kumi sasa, tangu Marc Vivien Foe atutoke..
Miaka kumi iliyopita tarehe 26 ya
mwezi wa sita, familia ya soka duniani ilimpoteza moja kati ya viungo
bora kabisa kuwahi kutokea hasa barani Afrika.
Akiwa na urefu wa futi sita nukta mbili, mwenye umbo la miraba ya
wastani, mweusi, Kijana aliyetokea kwenye familia masikini kwenye kijiji
kimoja nje ya mji wa Younde kwenye kijiji cha
Nkolo nchini Cameroon, mwaka 1975.
Anaitwa Marc Vivien Foe alipewa tuzo ya kamanda wa taifa la Cameroon,aliyefia vitani.
Foe alizaliwa mwaka tarehe mosi ya mwezi wa tano mwaka 1975 Younde
Cameroon. Alianza soka akiwa na klabu ya daraja la pili ya Union Garoua
kabla hajahamia kwenye klabu ya Canon Yaoundé, moja ya timu kubwa nchini Cameroon alishinda mataji kadhaa.
Nyota ya Foe ilianza kung`aa tangu alipoitwa kwa mara ya kwanza
kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon mwaka 1993 na kisha
aliongeza umaarufu wake na kuwafanya wakala na makocha wa vilabu kadhaa
barani Ulaya kuanza kuitafuta saini yake mwaka 1994 kwenye fainali za
kombe la dunia kule nchini Marekani.
Sir Alex Ferguson
aliyekuwa kocha wa Manchester United mwaka 1998 aliwahi kwenda kufanya
mazungumzo maalumu na wakala wa Foe na kisha kuonana na Foe mwenyewe
lakini juhudi za kutaka kumsajili Foe zilishindikana baada ya kuvunjika
mguu wakati akifanya maazoezi na timu yake ya taifa kwenye fainali za
kombe la dunia nchini Ufaransa.
Licha ya kuvunjika miguu, bado Fergie aliwaambia viongozi wa United
kuwa angelipenda kumsajili Foe lakini dili hilo lilishindikana na Foe
alienda West United baada ya kupona majeraha yake kwa uhamisho ulioweka
rekodi kwenye klabu hiyo ya mashariki mwa jiji la London kwa Pound
milioni 4.2 kwa wakati huo.
Foe alihamia West Ham akitokea Lens ya Ufaransa alikodumu kwa miaka
minne. Pamoja na kusajiliwa kwa uhamisho mkubwa kwenda Uptorn Park, Foe
hakuwa na msimu mzuri chini ya kocha Harry Redknapp kwani baada ya msimu
mmoja na nusu alirejea ufaransa na kujiunga na timu ya Olympique
Lyonnais au Lyon kama inavyofupishwa ambako alidumu kwa misimu miwili
kabla ya
Kevlvin Keegan kocha wa wakati huo wa Manchester City hajaamua
kumsajili na kumfanya mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha Man City.
Akiwa Man City Foe huenda Mungu ndo alikuwa akiionyesha dunia kilivyo
kipaji cha Marc Vivien Foe mtu anatejwa kuwa na moyo wa huruma na wa
kipekee, Alianza msimu vizuri na kufanikiwa kufunga magoli mengi na
muhimu kwenye mechi ngumu.
Moja ya vitu ambavyo Mashabiki wa Man City hawatoweza kuvisahau ni goli lake la mwisho kwenye uwanja wa Maine Road maarufu kama Wembley ya Kaskazini, uwanja wa zamani wa Manchester City kabla ya hawajahamia kwenye uwanja wa City of Manchester au Etihad.
Foe alifunga bao hilo kwenye mechi dhidi Sunderland ambapo City walishinda 3-0.
Kifo cha Marc Vivien Foe kiliishitusha dunia ya wapenda kandanda,
kwani ilikuwa ni ghafla sana. Ilikuwa ni kwenye michuano ya kombe la
mabara kama hii inayoendelea nchini Brazil hivi sasa, hatua ya nusu
fainali wakati Cameroon wakicheza na Colombia dakika ya 72, Foe
alidondoka katikati ya uwanja na juhudi za kwenda kuokoa maisha yake
zilifanyika kwa zaidi ya dakika 40 lakini zilishindikana.
Mashabiki wa soka, wachezaji na kila mkereketwa wa mpira wa miguu
duniani alituma na salamu za rambirambi kwa namna ya kipekee. Thiery
Henry nahodha wa wakati huo wa Ufaransa alishangilia goli lake kwenye
mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano hiyo kwa kuonyesha vidole juu
kama ishara ya kumkumbuka Foe, ambapo kabla ya mchezo huo wachezaji
wengi walitokwa na machozi kwa kumpoteza Foe.
Wachezaji wa Cameroon walioingia fainali ya michuano hiyo, walicheza
wakiwa na majonzi kwenye mechi ya fainali, Nahodha Ligobert Song na
Samwel Eto`o waliongoza timu hiyo kwa kubeba picha ya Foe na kusimama
kwa dakika moja uwanjani kuomboleza.
Marc Vivien Foe alifariki kwa kile ambacho madaktari wanakitaja kama
mshituko wa moyo. Nchini Cameroon Foe alipewa mazishi ya kitaifa na
heshima zote, ambapo Serikali ilisimamia gharama zote.
Manchester City ilitenga eneo maalumu kama bustani kwenye uwanja wao
zamani wa Maine Road kama ishara ya kumkumbuka Foe na kutangaza
kutoitumia jezi namba 23 ambayo Foe alikuwa akiivaa klabuni hapo,
kitendo ambacho kinaendelezwa hadi leo.
Lyon waliiweka jezi yake namba 17 kwa muda miaka kadhaa bila kuitumia
lakini, baadaye jezi hiyo ilikuja kupewa kiungo wa timu ya taifa ya
Cameroon Jean II Makoun.
Ni miaka kumi sasa tangu Foe aondoke duniani, akiwa ameacha mjane
binti mdogo wa wakati huo Marie-Louise ambaye aliachiwa jukumu la kulea
watoto watatu peke yake, wawili wakiume na binti mdogo ambaye baba yake
aliondoka duniani akimuacha akiwa na miezi na miwili.
Swali kubwa ambalo limekuwa likiendelea kuulizwa hata nchini Cameroon
ambako Foe alikuwa akitoa mchango mkubwa hasa kijijini kwake kwa
kusaidia kusomesha vijana, kusaidia wazee, kutoa misaada kwa watoto
yatima ni namna ambavyo familia yake imetunzwa na ilinufaika baada ya
kifo chake.
Inaelezwa Manchester City ilikuwa na mkataba wa mkopo na Foe, lakini Olympique Lyon ilishindwa kuilipa familia ya marehemu fedha zilizosalia kwenye mkataba wake, jambo ambalo ukweli wake haujulikani mpaka leo.
Samwel Eto`o alijitolea kuilea familia ya Foe huku akitoa tuzo na
fedha za zawadi zake mara kadhaa kwenda kwa familia ya Foe na watoto
wake.
Shirikisho la kandanda duniani FIFA, limekuwa karibu na familia ya
Foe ambapo mwaka 2009 kwenye mechi ya fainali ya kombe la shirikisho
mwana wa kiume wa Foe ambaye alikuwa na miaka 14 alitoa hotuba fupi
kuhusu kumbukumbu ya kifo cha baba yake.
Nchini Ufaransa kuna mfuko maalumu wa kusaidia watu wenye matatizo ya
moyo kwa kumbukumbu ya Foe, ambapo mjane wa Foe Marie-Louise ndiye
mlezi wa mfuko huo.
Licha ya kuondoka duniani miaka 10 iliyopita, Bado dunia hasa bara la
Afrika linaendelea kukumbuka kifo cha Marc Vivien Foe hasa umuhimu wake
kwa timu ya Cameroon ambayo ilikuwa imesheeni nyota wengi waliopa
mafanikio makubwa timu hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo Cameroon
imekuwa timu ya kawaida kwenye soka la Afrika na dunia ambapo hata
kwenye viwango vya FIFA imepitwa kwa ubora na timu ya taifa ya Tahiti.
Mashabiki wa Manchester City walisema “A Lion Never Die, He Just Lays There Sleeping” Kwa maana Simba huwa hafi, analala tu chini kupumzika.
Mungu aiweke Roho ya Marc Vivien Foe mahala panapo Stahili, Ameen.
No comments:
Post a Comment