MADHARA ya vurugu za kisiasa mkoani Arusha zinazodaiwa
kusababishwa na polisi kukabiliana na wafuasi wa vyama vya upinzani,
zimesababisha pigo kubwa kiuchumi katika ziara ya Rais wa Marekani,
Barack Obama, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Pigo hilo ambalo limesababisha serikali na mahoteli ya kitalii mkoani
humo kukosa mabilioni ya fedha, limetokana na hatua ya rais huyo na
ujumbe wake kufuta ziara yake kwenye mbunga za wanyama za Serengeti na
Mikumi.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni pigo kwa serikali ambayo ilitarajia
kuingiza mabilioni ya fedha baada ya rais huyo maarufu duniani na ujumbe
wake wa watu 700, kuzuru kwenye hifadhi hizo za taifa.
Rais Obama ambaye alianza ziara yake barani Afrika nchini Senegal,
alipata fursa ya kutembelea sehemu za utalii na hata alipokuwa nchini
Afrika Kusini, alitembelea sehemu ya utalii, hususan gereza alilopata
kufungwa Rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo, mzee Nelson Mandela, ambaye
kwa sasa yu mahututi.
Habari kutoka ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa zilisema Rais Obama ambaye anatarajiwa kuwasili kesho nchini,
akitokea nchini Afrika Kusini, amefuta ziara hizo kwa sababu za
kiusalama, hususan hali tete iliyoko mkoani Arusha.
Kwa mujibu wa habari hizo, hali tete ya Arusha, imesababisha mikutano
mingine mikubwa ya kimataifa kufanyika jijini Dar es Salaam.
Jiji la Dar es Salaam linatarajiwa kuwa na wageni 2,700, wakiwamo
wajumbe 800 kutoka nchi mbalimbali duniani, wanaohudhuria mkutano wa
Majadiliano ya Kimataifa kwa Manufaa ya Wote (ISPD), 2013. Mkutano huo
unafanyika katika ukumbi mpya wa kisasa wa Mwalimu Nyerere.
Umewahusisha
marais tisa, marais wastaafu watano na wakuu wa serikali.
Mbali ya ujio wa Rais Obama na ujumbe wake wa watu 700, serikali pia
inatarajia kupokea wajumbe wengine wa mkutano wa wake za marais barani
Afrika. Mikutano yote hiyo itafanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya maofisa wa wizara hiyo ambao waliomba majina yao
yahifadhiwe, waliliambia gazeti hili kuwa, katika hali ya kawaida
mikutano hiyo ingefanyika mjini Arusha ambako kuna hali ya hewa ya
baridi inayofanana sana na maeneo waliyotoka wageni wengi.
Wameeleza kuwa mandhari na ufinyu wa Jiji la Dar es Salaam kumeifanya
serikali mara nyingi kufanya mikutano mikubwa ya kimataifa jijini Arusha
ambako pia kuna hifadhi za utalii.
“Haya ni madhara ya kucheza na amani, hatutaki kunyoshea kidole mtu
yeyote, lakini sote tunahusika katika hali hiyo. Tunaweza kuilaumu
serikali, polisi na vyama vya siasa, lakini ni sote,” alisema mmoja wa
viongozi wa wizara hiyo.
Akizungumzia kufutwa kwa ziara ya Rais Obama kwenye hifadhi za taifa,
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema Rais
Obama hakuwa na mpango wa kwenda Serengeti bali alitaka kwenda Mikumi.
“Ni kweli amefuta ziara ya kwenda Mikumi, lakini hakuwa na mpango wa
kwenda Serengeti na si kwa sababu za kiusalama,” alisema Waziri
Kagasheki.
Matukio makubwa ya milipuko ya mabomu iliyotokea hivi karibuni mkoani
Arusha, moja katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi
Parokia ya Olasikiti na jingine kwenye mkutano wa hadhara wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku polisi ikishindwa kuwanasa
watuhumiwa, yameitia doa serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Katika mlipuko wa bomu la hivi karibuni katika mkutano wa hadhara wa
CHADEMA, zaidi ya watu wanne wamepoteza maisha huku mawaziri wa serikali
wakionekana dhahiri kuinyoshea kidole CHADEMA, huku CHADEMA
wakiinyoshea kidole serikali na Chama chake Cha Mapinduzi (CCM) kwamba
wanahusika.
Kishindo cha ujio wake kesho
Ukiachia kasoro hiyo, maandalizi ya ujio wa rais huyo yamekamilika.
Rais Obama, anatarajiwa kutua kesho saa 8:40 mchana, huku maofisa wa
Marekani wakilazimika kushika majukumu yote katika uwanja huo, ikiwamo
kuongoza ndege, ukaguzi wa abiria na mizigo.
Kazi ya kuongoza ndege ambayo kwa kawaida hufanywa na Mamlaka ya Anga
Tanzania (TAA), kesho kazi hiyo itasimamiwa na Wamarekani wenyewe.
Hata idadi ya maofisa wa Tanzania wakiwamo viongozi watakaompokea Rais Obama siku hiyo pia itapangwa na Wamarekani wenyewe.
Wakati huduma ya zimamoto ikiwa inahitajika zaidi wakati ndege
inapotua au kupaa, maofisa wa usalama wa Marekani wamekataa kutumia
zimamoto wa Tanzania.
Tayari magari 150 ya msafara wa ziara yake yamewasili nchini, huku
serikali kwa kushirikiana na makachero wa Marekani wakifanya mchujo wa
majina machache ya mawaziri watakaoruhusiwa kumpokea kiongozi huyo
maarufu zaidi duniani.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Moses Malaki,
aliliambia gazeti hili jana kuwa matayarisho ya ujio wa rais huyo
hayajapata kutokea nchini.
Tanzania Daima Jumapili ambayo jana ilikuwa ikipita katika maeneo
mbalimbali ambayo Rais huyo atapita, imeshuhudia kuwapo kwa ukaguzi wa
hali ya juu ukifanywa na makachero wa Marekani katika kuimarisha
ulinzi.
Wamarekani wameamua kufanya kila kitu wenyewe, kwa kuwa hawamwamini mtu yeyote, wakiwamo maofisa usalama wa Tanzania.
“Mazoezi haya yatatoa picha rasmi ya jinsi rais huyo atakavyotua, wapi
bendi ikae, wapi maofisa wasimame, wapokeaji na msafara wake mzima,”
alisema.
Kinachoendelea ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu
Nyerere ni mazoezi ya kumpokea Rais Obama, hususan jinsi watu
wanavyotakiwa kujipanga.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,
alisema wakati huu wa ujio wa Obama ulinzi ni mkali na wa kutisha kwa
wahalifu.
Alisema mtandao mkubwa wa askari umeshawekwa tayari barabarani
kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama ilivyopangwa hadi siku ya tukio
lenyewe ambayo ni kesho.
Mitaani ni Obama, Obama
Kila mtaa au kundi la watu unalokutana nalo jijini Dar es Salaam,
mazungumzo ni Rais Obama na ujio wake, hususan maandalizi yanayofanywa.
Wafanyabiashara ndogondogo ndio waathirika wakubwa wa ziara hiyo ambao
wengi waliozungumza na gazeti hili wamesema pasipo kumng’unya maneno
kwamba wamekerwa na ziara hiyo.
Wapo wananchi hasa waliojiajiri ambao wamepanga kutofika katikati ya
jiji kesho kuendelea na shughuli zao kwa hofu ya kuwapo vurugu hasa za
msongamano wa magari kwani baadhi ya barabara zitafungwa kabisa.
Mandela afunika ziara ya Obama
Kutoka nchini Afrika Kusini, inaelezwa kuwa ziara ya Rais Obama
imefunikwa na hali mbaya ya afya ya Rais mstaafu wa nchi hiyo, Nelson
Mandela.
Maelfu ya wananchi wa taifa hilo wameendelea kufurika katika hospitali
anakoendelea kupata matibabu mjini Pretoria na kuweka kando ujio wa
Rais Obama.
Via Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment