IMEELEZWA kuwa Tanzania inaongoza kwa vifo vya watoto
vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa, kwa nchi za Afrika Mashariki
huku kwa Afrika ikiwa ni ya tatu.
Mbali ya kuwa ya tatu katika Afrika baada ya nchi ya Nigeria na
Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo (DRC) pia ni miongoni mwa nchi 10 zenye
idadi kubwa ya vifo vya watoto vinavyotokea siku ya kwanza ya kuzaliwa
ulimwenguni kote.
Taarifa hiyo imetolewa jana na Mshauri wa Programu ya Afya wa Save
the Children nchini Tanzania Stephen Ayella wakati akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Ayella alisema Tanzania inachangia asilimia 2 ya vifo vinavyotokea
siku ya kwanza ya kuzaliwa ulimwenguni, ambavyo huchangiwa zaidi na
matatizo ya uzazi kabla ya muda wa kujifungua.
Alitaja sababu zingine kuwa ni ukosefu wa vifaa vya kujifungulia na
changamoto za kupata huduma kwa watoto wachanga, hususan kwa kina mama
wanaoishi maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa katika ripoti ya hali ya afya ya mama na mtoto ya
mwaka 2013 Tanzania imefanya mabadiliko makubwa ya kisera katika kupanua
huduma za afya kwa watoto wanaozaliwa.
Ayella alisema kuwa watoto milioni 1 hufa kila mwaka katika siku yao
ya kwanza ya kuzaliwa ama kwa lugha nyingine watoto wawili hufa kila
dakika, hivyo kuifanya siku ya kwanza kuwa siku ya hatari zaidi kwa
maisha ya wa watoto hao wanaozaliwa.
No comments:
Post a Comment