SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amemuagiza Mbunge wa Kuteuliwa,
James Mbatia (NCCR - Mageuzi), kuandika maelezo kuhusu aina ya sumu
anayoizungumzia kuwa inatokana na upungufu uliomo kwenye vitabu vya
Hisabati kwa shule za msingi ambayo inachangia kuua elimu ya Tanzania.
Makinda alitoa agizo hilo bungeni mjini hapa jana muda mfupi baada ya
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, kumaliza kujibu
swali la mbunge huyo wa kuteuliwa.
“Uandike maelezo na uyapeleke ukiwa umeeleza hiyo sumu inafanana
fananaje ...kwani kauli ulizozitoa kuhusiana na sumu ni nzito sana,”
alisema Makinda.
Mbunge huyo katika swali lake la nyongeza alitaka kujua kama serikali
iko tayari kupiga marufuku vitabu hivyo kuendelea kutumika kwa kuwa ni
sumu kutokana na miongozo yake kutofaa kwa taifa.
Pia mbunge huyo alitaka kujua mpango wa wizara kuwawajibisha watendaji.
Awali katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kujua kama vitabu
hivyo vya Hisabati vilihaririwa na wataalamu wa somo husika na kama
wataalamu hao hawakuweza kubaini udhaifu huo au kama ulionekana
walichukua hatua gani.
“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu
cha South Carolina (USA), chini ya ufadhili wa USAID iliandika vitabu
vya Hisabati kwa shule za sekondari, vitabu ambavyo havikuandikwa kwa
ubora unaokubalika, hii ikiwa ni sababu mojawapo kubwa inayosababisha
wanafunzi wengi kufeli somo la Hisabati,” alisema Mbatia.
Akijibu swali la nyongeza, Waziri Kawambwa alisema si kweli kabisa
kwamba vitabu hivyo ni sumu na vinaharibu elimu ya Tanzania na ndivyo
vinavyosababisha somo la hesabu kutosomeka.
Kawambwa alisema kazi ya kuhakiki vitabu hivyo ilifanyika kitaalamu
na kiusahihi na wataalamu wa wizara na kubaini kuwa vitabu hivyo vina
uwezo wa kutosha.
Kuhusu suala la kuwawajibisha wataalamu kwa madai kuwa wametoa majibu
ya uongo waziri alisema hiyo ni taarifa ya kikazi hivyo wataifanyia
kazi.
Akijibu swali la msingi, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Philipo Mulugo, alisema mwaka 2009 Rais Jakaya Kikwete aliomba msaada wa
vitabu vya Sayansi na Hisabati kutoka Serikali ya Marekani.
Alisema Serikali ya Marekani kupitia Shirika la USAID ilitoa msaada
huo chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Carolina ya Kusini
ambacho kilisimamia na kuratibu msaada huo.
“Wakati huo huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilikuwa imekwisha
kupata msaada huo mwaka 2009 kwa masomo ya Sayansi na Hisabati hususan
katika uandishi wa vitabu,” alisema.
Mulugo alifafanua kuwa wizara hiyo ilikubaliana na Chuo Kikuu cha
Jimbo la Carolina na Shirika la USAID kutumia vitabu ‘Mathematics for
Secondary School Book 1,2,3 na 4’.
Aidha, alisema wizara iliteua wataalamu sita wa somo la Hisabati ambao
walifanya kazi ya kuvihariri vitabu hivyo mwaka 2010, na baada ya kazi
hiyo, jukumu la kuvihakiki na kuvitathmini lilitekelezwa na watathmini
ambao ni walimu watatu wa somo la Hisabati kutoka shule za sekondari,
mtaalamu mmoja kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania na mshauri mmoja kutoka
Chuo Kikuu cha Jimbo la South Carolina.
Alisema kazi hiyo ilipokamilika wizara kupitia EMAC ilivipitisha na
kuvipa hati ya ithibati kuwa vitabu vya kiada katika shule za sekondari
Mei, 2011.
No comments:
Post a Comment