WADAU mbalimbali wa sekta ya elimu nchini wameikosoa bajeti ya
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, iliyosomwa jana bungeni mjini
Dodoma na kusema haina mwelekeo wa kutatua matatizo ya elimu yaliyoko
nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana wadau hao walisema kuna mambo
mengi hayajapewa kipaumbele kuweza kukwamua sekta nzima ya elimu.
Miongoni mwa wadau hao ni Mkurugenzi wa Haki Elimu, Elizabeth
Missokia, ambaye alisema licha ya wadau kuonyesha njia ya kukwamua sekta
ya elimu serikali haikujishughulisha kuyafanyia kazi mawazo hayo katika
bajeti yake.
Aliyataja mambo ambayo hayakutiliwa mkazo kuwa ni kuwajengea uwezo walimu pamoja na suala zima la lugha.
Msokia alisema bajeti haikutoa njia za kutatua changamoto mbalimbali
kama vile ununuzi wa vifaa mashuleni, vitabu na ujenzi wa maabara
sambamba na maboresho ya posho na mishahara ya walimu.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Dk. Kitila Mkumbo, alisema bajeti haijatenga fedha zozote kwa ajili ya
wanafunzi wa vyuo vikuu kufanya utafiti jambo alilosema ni hatari kwa
taifa kwa kile alichoeleza kuwa kila kukicha elimu ya juu inashuka.
“Hii haijajibu kiu ya watu wengi ambao walitaka kujua sababu za kufeli
kwa wanafunzi lakini mimi naamini kuwa kuna mambo mawili tu ikiwa ni
pamoja na kutokuwa na motisha kwa walimu wala mishahara inayoeleweka kwa
kuwa walimu ndio wanaolipwa mishahara midogo sana,” alisema Dk. Mkumbo.
Alisema hotuba ya bajeti haijaonyesha wizara imejifunza nini kutokana na matukio yaliyopita.
Naye mwakilishi kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) Antony
Mwakibinga alisema kuwa tatizo la serikali ni kutojifunza kutokana na
makosa na kuweka mikakati mbalimbali ya muda mrefu ili kuweza kuikomboa
elimu.
No comments:
Post a Comment