IMEELEZWA kwamba Watanzania wote wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya mabusha na matende.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Dk. Edward Kirumbi wakati
wa semina kwa wahariri na waandishi wa habari kuhusu uelewa wa magonjwa
yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Katika semina hiyo pia wataalamu wa magonjwa hayo walisema wakazi wa
majiji ya Mwanza na Dar es Salaam watapewa dawa za magonjwa hayo kwa
siku tano mfululizo kuanzia Juni 22, mwaka huu.
Aliyataja baadhi ya magonjwa sugu yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kuwa
ni mabusha na matende, minyoo, kichocho, usubi, trakoma na kichaa cha
mbwa ambayo husababisha ulemavu wa kudumu.
Dk. Kirumbi alisema maradhi hayo huenezwa na mbu aina ya Anopheles na
Curex ambao hubeba vimelea vya minyoo hivyo kuwaweka Watanzania wote
kwenye hatari hiyo bila kujali umri.
“Mbu anayekuambukiza malaria anaweza kukuambukiza mabusha au matende
kwa sababu yanaambukizwa kwa minyoo midogo midogo iliyopo kwenye mfumo
wa majimaji na damu,” alisema na kuongeza watu zaidi ya bilioni moja
wapo kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa hayo.
Awali, Dk. Upendo Mwingira, alisema Watanzania milioni 2.5 wapo
kwenye hatari ya kupata maambukizi ya trakoma huku akisisitiza kwamba
magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yapo zaidi kwenye jamii
maskini.
“Kwa vile yapo kwenye jamii maskini zaidi kwenye ukanda wa tropiki,
mgonjwa hana sauti, yanaathiri ukuaji wa mtoto kiakili, yanazorotesha
shughuli za maendeleo na kuzidisha umaskini,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Upendo ambaye pia ni Mratibu wa Mpango wa Taifa wa
kutokomeza magonjwa hayo (NTDCP) wamezifikia halmashauri 97 ambazo
huzipatia dawa kila mwaka.
“Tunao mpango wa kwenda kwenye halmashauri nyingine kwa kuongeza
majiji ya Dar es Salaam na Mwanza kwenye mpango wetu wa kugawa dawa
mara moja kila mwaka hivyo tunaamini tutazifikia halmashauri zaidi ya
105,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment