WANANCHI wa kijiji cha Hungumalwa kata ya Hungumalwa, wilaya ya
Kwimba, mkoani Mwanza, wameshutumu Diwani wa kata hiyo, Shija Malando
(CCM), na Ofisa Mtendaji wa kijiji, Johansen Malifedha, kuhujumu fedha
za miradi ya maendeleo.
Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamemtaka Mkuu wa Wilaya ya
Kwimba, Seleman Mzee, kwenda kijijini hapo Jumatatu ijayo, ili
akaelezwe tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Wakizungumza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya
shule ya msingi, Ng'washikuga, wananchi hao walidai mtendaji Malifedha
na diwani huyo wanashiriki kuhujumu fedha za maendeleo.
Walidai kuwepo kwa hujuma za miradi ya soko, stendi ya magari katika
eneo lililowekwa miaka mingi iliyopita, na kwamba kwa sasa miradi hiyo
imehamishiwa maeneo mengine kinyemela bila wananchi kushirikishwa.
“Huyu Ofisa Mtendaji hatumtaki hapa aondoke. Kwa nini anang’ang’ania
kwenye kijiji chetu? Sisi wananchi wa Hungumalwa hatutaki viongozi
wabovu,” walisikika wakisema wananchi hao.
Ofisa mtendaji huyo wa kijiji cha Hungumalwa, Malifedha alipoulizwa
kuhusiana na tuhuma hizo, alisema hazina ukweli wowote bali
zimepandikizwa na viongozi watatu wa kata hiyo ili afukuzwe kazi
kijijini hapo.
"Kwanza mpaka sasa hivi maisha yangu yako hatarini. Hivi karibuni
nimelishwa sumu, na nilihangaika nayo kwa siku tatu. Kwa hiyo msimamo
wangu itanibidi niondoke kwenye kijiji hiki ili kuokoa maisha yangu,"
alisema Malifedha.
Naye Diwani wa kata hiyo, Malando, alikanusha kuhusika na ubadhirifu
wa fedha zozote za umma, na kusema fedha za miradi ya vijiji
zinasimamiwa na viongozi wa serikali ya vijiji husika, na wala yeye si
mjumbe wala muweka saini kwenye akaunti ya benki.
“Tuhuma hizo ni njama tu ambazo zimepandikizwa kisiasa. Mimi kwanza
siyo mjumbe kwenye serikali za vijiji na wala si muweka saini kwenye
benki. Sasa hizo fedha nachukuaje?” alihoji.
No comments:
Post a Comment