WADAU mbalimbali wa soka hapa nchini, wamechukulia kwa sura
tofauti uteuzi wa Kamati mpya za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
uliofanywa juzi, baadhi wakiunga mkono na wengine wakihoji mamlaka ya
kufanya hivyo ilhali katiba ikiwa bado haijapitishwa na msajili.
Wengi wa wadau hao wameelezea kufurahishwa na kuachia ngazi kwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani, Idd Mtiginjola, na yule wa Kamati ya
Uchaguzi, Deo Lyato, wakidai ndizo zilizoibua mgogoro uliosababisha
hadi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kuingilia kati na kuagiza
marekebisho ya katiba.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mdau John Jambele alisema,
Rais wa TFF, Leodegar Tenga, ameanza kukubalika na kufuata haki
kimichezo kwa kukubali kujiengua Mtiginjola ambaye alionekana kuharibu
soka kutokana na utendaji wake ambao ilifikia hadi kuja kumpinga na
Tenga mwenyewe alipomtaka kufanya mapitio ‘Review’ ya wagombea
waliokata rufaa.
Alisema ana imani kubwa majaji na mawakili walioteuliwa katika kamati
hizo watafanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu, kutokana na kuwafahamu
ipasavyo katika utendaji kazi wao, kwani hawawezi kukaa katika magenge
na kujadili nani aenguliwe na nani apite wakati hawana vigezo.
“Tenga na kamati yake nawapongeza sana, kwani wamefanya suala zuri
sana, kukubali kukaa pembeni kwa Mtiginjola, huyo Lyato yeye
ilijulikana tu kwa kuwa sio mwanasheria na kamati yake ya uchaguzi
ilihitaji mwanasheria, hivyo basi nina imani watatenda haki hao
walioteuliwa sasa, kwa kuwa majaji hao nimekaa nao sana na nawajua,”
alisema Jambele.
Naye Michael Wambura alisema kuwa huu haukuwa muda muafaka kwa sasa
kutangaza kamati hizo wakati bado marekebisho ya katiba bado
hayajapitishwa na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo na hata serikali
pia.
“TFF, sijaona haraka waliyonayo, kwani bado katiba haijapitishwa
mpaka sasa, wangesubiri kwanza msajili na serikali wakubaliane na
marekebisho yao, halafu ndo watangaze hizo kamati zao, kwa mimi bado
naona ni ubabaishaji, kwani hata hizo zitakuwa kama yale yale
yaliyofanyika mwanzo,” alisema Wambura.
Kwa upande wake, Mussa Peter, aliwataka wote walioteuliwa katika
kamati hizo, kutenda haki ili waweze kuwapata viongozi bora hapo
baadaye, ambao watasaidia soka hapa nchini kukua na sio ubabaishaji
uliopo sasa.
Wakati wadau hao wakinena hayo, Rais wa TFF, Leodegar Tenga, ametoa
salamu za shukrani kutokana na utumishi wa Lyato uliotukuka akiwa
madarakani.
Akizungumza kwa niaba ya Tenga, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah,
alisema rais huyo na shirikisho hilo, linapenda kumshukuru Lyato kwa
utendaji kazi makini uliochangia maendeleo ya soka nchini na kwamba
litaendelea kuyaenzi mema aliyofanya.
Angetile aliongeza kuwa chini ya Lyato, Kamati ya Uchaguzi ilifanya
mengi yaliyotukuka katika kusukuma mbele gurudumu la soka, licha ya
changamoto kadhaa ngumu, hivyo TFF itaendelea kushirikiana naye kwa
sasa atakapokuwa nje ya kamati hiyo.
Kwa upande wake Lyato, hakusita kuushukuru ushirikiano aliopata
kutoka kwa Tenga akiwa katika kamati mbalimbali, huku akitoa shukrani
kwa wajumbe wote na wadau wengine waliomwezesha kutekeleza majukumu
yake vema.
“Nimeridhia mabadiliko yaliyofanywa na kutangazwa na Rais Tenga na
kimsingi napenda kumshukuru kila mmoja kwa nafasi yake, katika miaka
yangu minane ya kufanya kazi ndani ya kamati tofauti za TFF toka mwaka
2005,” alisema Lyato.
Aliongeza kuwa shukrani zaidi ziwafikie wadau wote wa soka, wakiwamo
wajumbe wa kamati za Kuchunguza Mkasa wa Serengeti Boys, Kamati ya
Maendeleo ya Taifa Stars, Kamati ya Kuboresha Mapato ya TFF na Kamati
mbili za Uchaguzi (2009-11 na 2011-13).
Kamati ya Uchaguzi hivi sasa itakuwa chini ya uenyekiti wa Hamidu
Mbwezeleni huku Makamu akiwa ni Moses Kaluwa na wajumbe Mustafa Siani,
Hassan Dyamwale na Kitwana Manara.
Kamati ya Rufaa za Maadili itakuwa chini ya Jaji Steven Ihema
akisaidiwa na Victoria Makani huku wajumbe ni Mohamed Misanga, Henry
Tandau na Murtaza Mangungu, wakati Kamati ya Maadili ni Jesse Mguto
mwenyekiti, Francis Kabwe makamu mwenyekiti na wajumbe DCP Mohamed
Mpinga, Prof. Madundo Mtambo na Evod Mmanda.
No comments:
Post a Comment