WADHAMINI wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Kilimanjaro Premium
Lager, wamesema wana imani timu hiyo itafanya vizuri katika mechi ya
marudiano dhidi ya Uganda ‘The Cranes’ kuwania kufuzu Fainali za
Mataifa ya Afrika kwa Nyota Wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN), kwani
maandalizi ni mazuri.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kanda ya
Ziwa, Malaki Sitaki, wakati TBL Mwanza ilipowaandalia chakula cha jioni
wachezaji wa Stars.
Malaki aliishukuru TFF kwa kuichagua Mwanza tena iwe kambi ya Stars,
kwani wakaazi wa jiji hilo wanaipenda timu yao na wamekuwa wakijitokeza
kwa wingi kuangalia wachezaji wakiendelea na mazoezi chini ya Kocha
Kim Poulsen.
“Tuna imani mtafanya vizuri ili twende CHAN….kama Waganda walitufunga
bao moja kwetu, sisi tuna uwezo wa kuwafunga mawili kwao,” alisema
Malaki.
Alisema kocha amefanya kazi nzuri tangu aanze kuifundisha timu ya
taifa na anastahili pongezi kwa mafanikio aliyopata hadi sasa.
“Baadhi ya matunda tuliyoyaona ni kuwafunga vigogo kama Zambia,
Cameroon na Morocco,” alisema na kuongeza kuwa Kilimanjaro Premium
Lager iko pamoja na Stars, kwani ushirikiano uliopo ni wa manufaa kwa
pande zote.
Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, aliipongeza
Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwa karibu na Taifa Stars wakati wote.
Alisema matokeo ya awali ya Stars kufungwa bao moja yasiwakatishe
wachezaji na wananchi tamaa, kwani kilichotokea ni matokeo ya mpira na
Stars inaweza kugeuza meza ikiwa Kampala.
Alisema Stars ilivyopiga kambi Mwanza mwaka jana kabla ya kwenda
kwenye mashindano ya CECAFA ilishinda mechi tatu mfululizo kwa hiyo
wanaamini safari hii pia kutakuwa na matokeo mazuri Kampala Jumamosi
Julai 27, Stars itakapocheza na Cranes katika mechi ya marudiano.
Naye Poulsen alisema wachezaji wako katika hali nzuri na ana imani watafanya kazi nzuri Kampala.
No comments:
Post a Comment