WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amevitaka vyombo vya
dola na wafanyabiashara wakubwa nchini, kujenga mahusiano bora kati yao
na wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) ili kuondoa tabaka la
matajiri na masikini linaloweza kuathiri uchumi wa taifa.
Lowassa aliyasema hayo jana wakati akizungumza na machinga wa eneo la
Makoroboi jijini Mwanza, ambao pamoja na mambo mengine aliwachangia sh
milioni 20 kwa ajili ya kutunisha mfuko wao.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliinyoshea kidole
Serikali ya chama chake cha Mapinduzi (CCM) na kuitaka ihakikishe
inatekeleza kwa vitendo ilani yake inayosisitiza wananchi kuwezeshwa
kiuchumi ili kuondoa matabaka.
Huku akishangiliwa na wafanyabiashara hao, Lowassa ambaye aliongozana
na baadhi ya makada wa CCM kutoka ndani na nje ya Mwanza, alisema kila
mwananchi wa Tanzania lazima ale, ingawa kwa namna tofauti.
Alisema kuwa ili amani iwepo nchini, lazima Jeshi la Polisi na wafanyabiashara wakubwa wawathamini wafanyabiashara wadogo.
“Tunataka tuwasaidie hawa vijana wetu, maana ni nguzo kubwa sana
katika maendeleo ya taifa. Ilani ya CCM inasema lazima watu wawezeshwe
kiuchumi.
“Kwa maana hiyo katika nchi yetu kila mtu lazima ale. Na kula
kwenyewe tunatofautiana, huyu anakula mkate na huyu anakula hiki. Na
ili amani iwepo lazima RPC au OCD na wafanyabiashara wawathamini
machinga,” alisema Lowassa.
Pia alitahadharisha kuwa endapo wafanyabiashara hao wadogo
watadharauliwa katika nchi, lazima watakula sahani moja na matajiri.
Alitumia pia fursa hiyo kukanusha tuhuma dhidi yake kwamba amejilimbikizia mali.
“Wapo baadhi ya watu wanasema hela ninazotoa hizi ni zangu. Mimi sina
fedha, ninazotoa ninapewa na marafiki zangu. Mimi si tajiri wa fedha,
ila ni tajiri wa marafiki na ushawishi ninao,” alitamba.
Katika hatua nyingine, Lowassa alikataa kuulizwa maswali na
wamachinga hao akisema ameandaa kamati itakayoratibu harambee ya
kuwachangia kwa lengo la kupata sh bilioni moja.
“Kwa maandalizi ya harambee nitakayorudi tena kuifanya, na ili mjue
kwamba nipo makini natoa hundi ya sh milioni 10 na milioni 10 nyingine
nitaitoa leo hii,” alisema Lowassa ambaye baadaye aliondoka kwa
kutembea kwa miguu hadi Mwanza Hotel.
Habari na Tanzania Daima
nchi inaitaji kiongozi ambae ni mwepesi ,makini na asiye mwoga kuchukua atua na kufanya mamuzi.nchi haitaki kiongozi mwoga na anayewaonea aibu viongozi wenzake kuwajibisha pale wanapo halibu au kutenda kinyume na maelekezo ya bosi wake,huyo kiongozi hatufai kabisa katika taifa letu.
ReplyDelete