Kadri mjadala wa Rasimu ya Katiba unavyozidi kupamba moto,
wanasiasa wanazidi kubaini ufinyu wa nafasi zao iwapo rasimu hiyo
itapita bila mabadiliko, hivyo kulazimika kuibua vihoja na mambo ambayo
hawataki yawemo wakidhani kuwa yanaweza kuwaathiri.
Mada kuu katika rasimu iliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba inayoleta hofu kwa wengi ni muundo wa Muungano wa Serikali tatu. Muundo huu ndiyo unaotoa taswira ya hali ya kisiasa hapa nchini hapo baadaye, iwapo Katiba Mpya itapitishwa.
Miongoni mwa wanasiasa waliotikisika ni wanasiasa kutoka Zanzibar, hasa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hata wenzao wa bara ambao wameonyesha kila dalili za woga wa kupoteza madaraka.
Chama hicho kimeamua kutoa waraka wa ‘kuichana’ Rasimu ya Katiba, kikipinga Serikali tatu na mambo mengine mengi yanayopendekezwa.
Wanasiasa wenye mwelekeo huo wamejificha katika kivuli cha ‘gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali tatu’.
Kwa mfano, Samuel Sitta, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki anasema haijawahi kuwapo nchi yoyote duniani yenye marais watatu kama inayopendekezwa, kana kwamba ilishawahi kuwapo nchi yenye marais wawili kama iliyopo sasa, Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar katika nchi moja.
Deus Kibamba, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, anawashauri wanasiasa wanaopinga Serikali tatu kwa kigezo cha gharama kutafuta hoja nyingine, kwa maelezo kuwa hicho ni kihoja.
“Mimi nadhani Serikali tatu zitapunguza gharama. Ukiangalia ukubwa wa Serikali ya sasa ya mawaziri 60 ukalinganisha na Serikali inayopendekezwa ya mawaziri wasiozidi 15; wabunge wa muungano 75, ukiongeza wale wa Zanzibar na Tanzania bara, jumla yao haitaweza kufika ya sasa ya 357 (ukiondoa watatu ambao Rais Jakaya Kikwete hajateua). Hivyo gharama zitapunguzwa,” anasema.
Kibamba ambaye alikuwa anazungumza na Muungano wa Vikundi vya Wakulima (Mviwata) ambao wamejiunga kama Baraza la Katiba, anasema kwa jumla, pamoja na upungufu kadhaa yaliyomo, Rasimu ya Katiba ina mambo mengi mazuri.
Hata hivyo, anasema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoandaa Rasimu hiyo imevunja Katiba kwa kupendekeza kupunguza mambo ya Muungano kutoka 11 yaliyofikiwa mwaka 1964 hadi saba.
Rasimu hiyo ya Katiba imependekeza mambo ya Muungano yawe saba – Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Hata hivyo, Katiba ya sasa ina mambo ya Muungano 22 baada ya kuongezwa kwa nyakati tofauti kutoka 11, hatua ambayo imekuwa ikilalamikiwa na Wazanzibari wengine.
Nafasi ya mkulima
Vilevile Kibamba anasema kama ambavyo mkulima
amekuwa akipuuuzwa kwa namna mbalimbali, hata Rasimu ya Katiba
inayojadiliwa haijarejesha umiliki wa nchi, mikononi mwake, baada ya
kile kifungu cha
“Tanzania ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi” kuondolewa katika Katiba ya mwaka 1961.
“Rasimu hii haielezi nchi hii ni ya akina nani, pamoja na kutoeleza, mimi nadhani nchi hii kwa sasa ni ya wafanyabiashara na wawekezaji,” anasema Kibamba.
Pamoja na kuikosoa rasimu hiyo, Kibamba anasema
walau imeonyesha kuwa inaandaliwa kwa kuwashirikisha wananchi, wakiwamo
wakulima na wafanyakazi, na maandalizi yake yanafuata utaratibu wa
kisheria, hivyo Katiba itakayopatikana itakuwa halali.
“Katiba tano za mwaka 1961, 1962, 1964, 1965 na ya sasa ya 1977 zilikosa uhalali kwa sababu hazikuwasirikisha wananchi, wananchi walitakiwa wajifunze katiba baada ya kupitishwa,” anasema.
Anabainisha kuwa mawazo ya wakulima hao ni muhimu
ili haki zao ziweze kuingizwa, badala ya sasa ambazo ‘zimechomekwa’
katika makundi madogo wakati wenyewe ndio kundi kubwa.
Kwa mujibu wa Kibamba, wakulima hao wapiganie ardhi, rasilimali na misitu ambayo ni mambo muhimu kwa wakulima, ili yaweze kuingizwa katika rasimu, badala ya kuishia kuyaona kama mambo ambayo si ya Muungano.
Ushauri wa Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye anawataka
kutumia wingi wao na baraza lao la katiba kuingiza mambo yenye masilahi
yao kwenye Katiba ijayo.
No comments:
Post a Comment