MAJADILIANO makubwa yameibuka kati ya vijana na viongozi wa
kidini, wakitaka viongozi hao wasiendelee na msimamo wao wa kupinga
matumizi ya kondomu kwa madai waumini wao wengi wanaangamia kwa ugonjwa
wa ukimwi.
Katika majadiliano hayo, vijana wanataka viongozi wao kutambua kwamba
kwa kipindi kirefu wamekuwa wakiwahubiria waumini wao kuacha zinaa,
lakini bado wanaendelea na na zinaa zinazochangia kuambukizwa virusi
vya ukimwi.
Balozi wa vijana, Suleiman Msei, alisema waumini wengi wamekuwa
wakionyesha maadili mazuri kwa viongozi wao, lakini baada ya kutoka
kanisani au msikitini wamekuwa wakifanya vitendo visivyo vya maadili.
Alisema ni vigumu kiongozi wa dini kutamka hadharani kuruhusu
matumizi ya kondomu, lakini kutokana na hali halisi vijana ambao ndio
waathirika wakubwa, wangeona vema kama elimu ya suala hilo isingewekewa
kipingamizi kwa kuwa wengi wameshindwa kumtii Mungu.
Akijibu hoja za vijana hao, Imamu wa Msikiti wa Barabara ya 10 jijini
Tanga, Mohamed Yahya, alisema kitendo cha kuruhusu matumizi ya kondomu
ni kuhamasisha zinaa kwa waumini suala ambalo linapingwa katika dini
zote.
“Sisi kama viongozi wa kidini tutazungumzia watu kuacha zinaa,
kuruhusu matumizi ya kondomu ni sawa na kuwafanya waumini tulionao
ambao ni waadilifu, nao kujihusisha na vitendo vya zinaa,” alisema
Imamu Yahya.
No comments:
Post a Comment