JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wametuhumiwa kuwa
kaburi la mapato ya viingilio vya mlangoni katika Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam jana na Katibu Mkuu wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah, wakati Balozi wa
China nchini, Lu Youqung, akikabidhi rasmi uwanja huo kwa Serikali ya
Tanzania.
Alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la watazamaji wanaoingia uwanjani
bila tiketi halali kutokana na uaminifu mdogo wa baadhi ya askari wa
jeshi hilo ambao wamekuwa wakiwapitisha watu hovyo na kujipatia fedha
licha ya kulipwa posho kwa kazi hiyo.
“TFF tumekuwa tukilaumiwa kutangaza mapato tofauti na idadi ya
watazamaji wanaoonekana uwanjani, jambo hili halituhusu sisi kwa kuwa
hiyo ni kazi tuliyoikadhi kwa askari 350, lakini pamoja na wingi wao,
bado watu wanaingia bila tiketi,” alisema Osiah.
Mbali ya kulinyooshea kidole moja kwa moja Jeshi la Polisi kuhusika na
kuingiza watu kwa njia za panya, Osiah amewataka watumiaji wote kujenga
utamaduni wa kulipa kiingilio halali.
“Tumewahi kuwakamata watuhumiwa kadhaa wakiwemo askari polisi, lakini
hakuna hatua walizochukuliwa, wanaachwa bila sisi kufahamu, pia hatuwezi
kuwashitaki Polisi kwa vile ni wao kwa wao,” alisema Osiah.
Osiah aliyasema hayo baada ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella
Mukangara, kukabidhiwa rasmi uwanja huo jana na
Balozi wa China, Youqung, baada ya ujenzi huo uliodumu kwa miaka saba.
Waziri Mukangara kwa upande wake, aliwasihi watumiaji wa uwanja huo
kwa mechi za soka, matamasha na matukio mengineyo kutoa takwimu sahihi
badala ya kufanya udanganyifu.
“Watumiaji wa uwanja huu kuanzia mechi za soka, mashindano mbalimbali
na matamasha, wanatakiwa kutoa takwimu sahihi za viingilio ili mradi wa
uwanja huu uwanufaishe wananchi wote.
Alisema licha ya uwanja huo kuwa na uwezo wa kuingiza watu 60,000,
hata ikitokea umejaza watu mapato yanayotangazwa hayaendani na wingi wa
watu walioufurika uwanjani.
“Tunapaswa kulinga na kujivunia uwanja wetu wa kimataifa ambao
utatuingizia mapato makubwa na kuinua uchumi wetu, kuongeza ajira na
kutuwezesha kuandaa mashindano makubwa ambayo yatakuza utalii wetu na
kuliletea sifa kubwa taifa letu,” alisema Mukangara.
Mukangara aliongeza kuwa umefika wakati wa Watanzania kujenga
utamaduni wa kulinda rasilimali yao kwa kuitunza na kuithamini hivyo
akasema anachukizwa na tabia ya baadhi ya mashabiki kuharibu miundombinu
ya uwanja huo ikiwemo kung’oa viti. Waziri huyo alisema kama Watanzania
wataujali uwanja huo unaweza kutumika kwa muda mrefu zaidi na kuwasihi
waache tabia ya kuchafua vyoo kwa makusudi na uharibifu mwingine wa
uwanja huo ambao ni mali ya wote.
Waziri Mukangara, aliishukuru Serikali ya China kwa mchango wao mkubwa
walioufanya akisema Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano kati ya
nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment