KATIKA kuhamasisha wanaume kujenga tabia ya kuwasindikiza wenza
wao kliniki, Halmashauri ya Nkasi, mkoani Rukwa, imeweka utaratibu wa
kuwatunukia vyeti maalumu wanaume wanaofanya hivyo.
Hayo yameelezwa na mratibu wa mradi wa ushiriki wa wanaume katika
afya ya uzazi wilayani Nkasi, Nestori Sendani, wakati akiwasilisha
taarifa kwa waandishi wa habari waliokwenda hivi karibuni kujionea
utekelezaji wa mradi huo kwa ufadhili wa Chama cha Uzazi cha Sweden
(RFSU).
Sendani alisema kutokana na hatua hiyo, idadi ya wanaume
wanaohudhuria kliniki imeongezeka kutoka 239 Januari mwaka huu hadi 520
Mei mwaka huu, ongezeko ambalo ni tofauti na walivyotarajia.
Mratibu huyo aliongeza kwamba tangu kuanza kutolewa kwa elimu,
wanaume wamebadilika kitabia tofauti na ilivyokuwa awali ambako suala
la kwenda kliniki lilionekana ni la kinamama peke yao.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kijiji cha Swahila, Kata ya Mkwamba,
Khamis Hassan, alisema tangu TMEP iingie kijijini hapo, imeongeza kwa
kiasi kikubwa upendo ndani ya familia, na akaomba waongezewe muda.
Alidai kwamba awali wakati mafunzo hayo ya ushiriki wa wanaume kwenye
afya ya uzazi yalipokuwa yakitolewa kituoni hapo, waliona kama
wanatukanwa kwa kuwa ni utamaduni ambao ulikuwa haujazoeleka.
Hassan alisema kuwa katika kufikisha elimu hiyo wamekuwa wakitumia
mbinu mbalimbali za kufikisha ujumbe ikiwemo kuwatumia wazee maarufu na
viongozi wa dini na pale mwanaume anapoonekana kumsindikiza mwenza
wake kliniki hupewa kipaumbele katika kuhudumiwa tofauti na mama
aliyekuja peke yake.
Karison Masebo, mwalimu wa Shule ya Msingi Swahila, alisema kupitia
mradi huo kesi za mimba mashuleni zimepungua kwa kiasi kikubwa. Kwa
mwaka jana walipata kesi tatu tu tofauti na huko nyuma ambako kila
mwaka wasichana sita hadi nane walikuwa wakifukuzwa shule kutokana na
kupata ujauzito.
Pia Masebo alisema kwa sasa vijana wamekuwa wazi kuelezea afya zao na
kwa wale wanaohitaji kondomu wamekuwa wakienda kuzichukua kwa
waelimishaji rika bila ya woga.
No comments:
Post a Comment